HabariSiasa

UhuRaila wakejeliwa kwa 'kutakasa ufisadi'

June 18th, 2020 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

USHIRIKA wa Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga chini ya mwavuli wa handisheki umetajwa kama unaolemaza vita dhidi ya ufisadi, huku ukionyesha ubaguzi katika kuandama wezi wa rasilimali za kitaifa.

Katika siasa zinazoendelea katika ung’atuzi wa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Rais na Bw Odinga wamekosolewa pakubwa kwa mapendeleo yao ya wazi ya kukinga baadhi ya washukiwa huku wakiwaandama wengine.

Hii ni baada ya bunge la Seneti kuonekana wazi kuwa lina mirengo miwili ya kisiasa ambayo inamenyana kumzamisha au kumnusuru Bi Waiguru, ule wa handisheki ukionekana wazi kuwa hauzingatii sana ushahidi wa bunge la Kaunti ya Kirinyaga bali unazingatia tu masilahi ya umoja wa Raila na Uhuru.

Tayari, mwandani wa Raila ambaye ni Seneta wa Siaya James Orengo ametangaza kuwa “kesi dhidi ya Waiguru haina msingi bali anawindwa kisiasa na mahasidi wa handisheki. Wanatafuta kichwa cha Waiguru!”

Naye kiranja wa wengi katika bunge hilo la Seneti Irungu Kang’ata ametangaza kuwa “mimi naunga mkono msimamo wa Rais wetu na kinara wetu wa chama cha Jubilee kuwa suala hili la Kirinyaga litatuliwe haraka ili kaunti hiyo itulie.”

Aliyekuwa Waziri wa masuala ya kikatiba na haki, Martha Karua amesema kuwa ushirika huo wa handisheki umepotoka kutoka nia njema ya kuleta amani na utengamano nchini na kugeuka kwanza kuwa mauti kwa demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa na hatimaye kuondoa ule uwajibikaji wa upinzani kuwa nyapara wa utawala wa serikali.

Bi Karua aliye pia kinara wa chama cha Narc-Kenya aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa kwa sasa hakuna uwezekano wa ushirika huo kuwafaa Wakenya na uchumi wao katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine ya kiutawala.

Alisema kuwa “wawili hawa wamekuwa wakidai kuwa idara ya mahakama ndiyo imekuwa kizingiti kikuu katika vita dhidi ya ufisadi, lakini kwa sasa ni wazi kuwa hata katika fikira na utendakazi wa wawili hawa, hata wao ni visiki katika vita hivi.”

Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa alisema kuwa kuna visa kadhaa ambapo akiwa mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu bajeti alipata shinikizo za kutengea miradi ghusi pesa za kimaendeleo kutoka mrengo wa Handisheki.

“Kuna wizara za mawaziri wa handisheki ambazo zilikuwa zinasukuma pesa za kimagendo kutengewa miradi yao…Mimi nilikuwa nikikataa na mojawapo ya miradi hiyo ya ukora ni kuhusu utapeli wa shamba la Ruaraka ambapo Wizara ya Elimu ikiwa kwa wakati mmoja mikononi mwa Dkt Fred Matiang’i  ambapo hadi sasa hakuna taasisi inayofuatilia kesi hii kwa kuwa huyu Matiang’i ni wa Handisheki,” akasema.

Ni msimamo ambao ulitiliwa mkazo na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen aliyesema kuwa “vita dhidi ya ufisadi kwa sasa ni silaha ya kisiasa mikononi mwa baadhi ya mirengo ya kisiasa.”

Amesema kuwa wale ambao humuunga mkono naibu wa Rais Dkt William Ruto wakisingiziwa ufisadi huwa wanasukumwa mbio hadi nje ya nyadhifa huku wale wa handisheki wakiwa sasa na idhini rasmi ya kutapeli, kufuja, kuiba na kufisadi watakavyo kwa kuwa wako katika kambi ya wadosi.

Alisema kuwa Raila amekuwa akijipendekeza kama mpiganiaji wa haki za Wakenya na utawala bora lakini “amegeuka kuwa wa kutakasa wale ambao wamehusishwa na ufisadi bora tu watangaze kuwa wanamuunga mkono.”

Alisema kuwa Raila ameambukiza Uhuru msimamo huo dhidi ya ufisadi ambapo “ukionekana kuwa unaunga mkono muungano wa handisheki bila masharti, unatakaswa katika idara za kuchunguza ufisadi.”

Katika hali hiyo, Murkomen aliteta kuwa watu wa Kirinyaga sawia na wengine ambao wako katika mirengo tofauti ya kisiasa waelewe kuwa “vita dhidi ya ufisadi ni kwa wale ambao watakataa kujumuishwa katika mrengo mmoja wa kisiasa hapa nchini kwa lazima.”

Aliyeandaa mswada wa kumng’atua Bi Waiguru katika bunge la Kirinyaga, Kinyua wa Wangui alisema kuwa “mimi sitaki kuhusika kamwe na ukora na unafiki huu ambao umeonekana katika bunge la Seneti.”

Alisema kuwa “ni wazi kuwa kumeandaliwa njama ya kutupuuza kama bunge la Kaunti na Uhuru na Raila wanafaa waelewe kuwa hata wakimwokoa Waiguru katika Seneti, bado atakuja hapa Kirinyaga na tutawafunza adabu za kutuheshimu.”

Kiranja wa bunge hilo la Kirinyaga Pius Njogu alisema kuwa “huu ni utawala wa giza, ushirikiano wa hujuma na uliojaa unafiki wa kupambana na vita dhidi ya ufisadi,” huku aliyekuwa kiranja wa wengi, Kamau Murango akisema kuwa “Uhuru na Raila hawajaonyesha nia ya kuwa na uwazi dhidi ya kupambana na ufisadi.”