HabariSiasa

Uhuru aagiza polisi waliohudumu kwenye Uchaguzi Mkuu walipwe marupurupu yao

March 13th, 2018 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta ameagiza Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinett kuhakikisha maafisa waliohudumu katika majukumu maalum kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2017 wamelipwa marupurupu yote kama walivyoahidiwa.

Hii ni kufuatia malalamiko miongoni mwa maafisa hao ambao licha ya kuahidiwa marupurupu ya kati ya Sh30,000 na Sh70,000 kutegemea na siku ambazo walifanya kazi, wamekuwa wakilipwa kati ya Sh6,000 na Sh30,000.

Wiki iliyopita maafisa hao walikataa kuchukua pesa hizo na wakatoa habari kwa vyombo vya habari wakitaka kujua sababu ya pesa hizo kupunguzwa.

Katika barua ambayo imetumiwa Bw Boinett na kunakiliwa kwa Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC) ikiwa imetiwa sahihi na Bw Kennedy Kihara kwa niaba ya rais, hali hiyo inafaa kurekebishwa mara moja.

“Maafisa wa polisi waliohudumu katika majukumu maalum ya maandalizi, ushirikishi na kulinda kura za uchaguzi wa Agosti 8, 2017 na Oktoba 26, 2017 walifanya hivyo kwa mujibu wa maelewano kuwa wangelipwa marupurupu kwa mujibu wa kanuni za utenda kazi wa idara ya polisi na kuidhinishwa na Tume ya Mishahara (SRC),” inasema barua hiyo.

“Ni msimamo wa rais kuwa malumbano hayo ambayo yanajitokeza katika kulipa marupurupu hayo hayafai katika kuimarisha imani na motisha ya maafisa wa polisi.

Uadilifu ni nguzo moja muhimu ya kusimamia maafisa wote wa serikali na ni matumaini ya rais kuwa hali hii itashughulikiwa kwa haraka na kwa kuzingatia uwazi,” barua hiyo inaeleza.

Barua hiyo ambayo ilitumwa Ijumaa wiki jana imezua taharuki miongoni mwa wakuu wa vitengo Polisi wa Kawaida, Polisi wa Utawala (AP), Idara za Magereza, Shirika la Huduma kwa Wanyama Pori (KWS) na Idara ya Misitu (KFS).

Duru zinasema kumetokea sintofahamu baina ya vitengo kutokana na Polisi wa Kawaida kuthibiti shughuli za kulipa marupurupu hayo.

Maafisa wa ngazi za chini wanalalamika kuwa imekuwa ni kawaida kwa wakuu wao kukosa kuwalipa marupurupu yao kulingana na makubaliano.

“Marupurupu hayo kwa kawaida yanafaa kujumuishwa kwenye mishahara yetu na kulipwa mwisho wa mwezi. Lakini hali hii ya wakubwa kutugaiwa pesa hizo kama njugu ndani ya ofisi zao ni njama ya kutuibia hadharani,” akasema mmoja wa maafisa hao.