Habari

Uhuru aahidi wapwani vinono

September 8th, 2019 2 min read

Na ANTHONY KITIMO na ALLAN OLINGO

KAUNTI zote sita za Pwani zitafaidika pakubwa baada ya Rais Kenyatta kuahidi kuanzisha na kutekeleza miradi kadha ya maendeleo eneo hilo.

Kwenye mkutano na viongozi wa Pwani katika Ikulu ya Mombasa, Rais Kenyatta pia aliahidi kuhakikisha kuwa miradi kadha iliyokwama na iliyonuiwa kuanzishwa katika kaunti hizo itatekelezwa..

Rais, ambaye aliandamana na Kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yattani, pia aliahidi kuwa serikali itawekeza katika miradi mingine kuhakikisha inakamilika katika kipindi kilichowekwa.

Mkutano huo, Taifa Leo ilifahamishwa, uliitishwa na viongozi wa Pwani waliotaka Rais kuzungumzia suala la kufufua uchumi wa kanda hiyo na hofu ya nafasi za kazi kupotea katika bandari ya Mombasa.

Duru zilisema kuwa Rais alitumia mkutano huo kufahamisha viongozi hatua ambazo zimepigwa kuhusiana na miradi mikubwa mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Kitaifa.

Taita Taveta pia ilinufaika pakubwa baada ya Rais Kenyatta kuahidi kuhakikisha itagawiwa mapato yanayokusanywa katika Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo ya ekari 10,000.

“Tumefurahi kwamba Rais alisikia maombi yetu na kuagiza mashauriano zaidi kati yetu na Shirika la Wanyamapori (KWS) kwa uongozi wa Waziri wa Utalii Najib Balala. Sasa wameondoka katika msimamo wao wa ‘hakuna mazungumzo’ na sasa wataketi mezani nasi,” Seneta wa Taita Taveta Johnes Mwaruma alieleza.

Rais pia aliahidi kuhakikisha miradi kadha ya barabara inakamilika ikiwemo ile ya Mwatate-Lumi.

Bw Mwaruma alisema: “Hizi ni habari njema kwa viongozi wa Pwani kwa sababu Rais alitilia mkazo kwamba atatimiza miradi hii yote. Tulikubaliana kuwa na kikao Sikukuu ya Mashujaa ili kufuatilia hatua ambazo zimepigwa.”

Kutatua shida ya mara kwa mara ya uhaba wa maji katika kaunti zote za Pwani, hususan mjini Mombasa, Gavana Joho alimhimiza Rais kuharakisha utekelezaji wa mradi wa Mzima Springs II wa Sh42 bilioni na ule wa Bwawa la Mwache na akakubali.

“Tulimuambia Rais kuharakisha utekelezaji wa masuala muhimu yanayoathiri watu wetu. Tumefurahi kwamba alitoa agizo kwa maafisa wake washughulikie masuala hayo,” akasema Seneta wa Mombasa Mohamed Faki.

Ujenzi wa bandari

Gavana wa Kwale Salim Mvurya pia aliomba kuharakishwa kwa ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Shimoni mjini Kwale, itakayogharimu Sh20 bilioni, na ambayo ikikamilika itachochea ukuaji wa kiuchumi eneo hilo. Rais Kenyatta pia aliidhinisha miradi kadha ya barabara katika Kaunti ya Tana River kama alivyoomba Gavana Dhado Godhana.

Rais alikiri kwamba Tana River imeachwa nyuma katika maendeleo, na kwamba inafaa kupewa kipaumbele hususan katika miradi ya miundomsingi. Kuambatana na hilo Bw Kenyatta aliahidi ujenzi wa uwanja wa ndege wa Dada na kukamilisha barabara ya Machakos-Kalalalani-Hola-Lamu.

Barabara hiyo ikikamilika itaunganisha kaunti ya Tana River na Nairobi na hivyo kupunguza safari ya kutoka jiji kuu hadi kaunti kwa kilomita zaidi ya 200.

Rais pia alisindkizwa na magavana, maseneta, wabunge kutoka maeneo bunge 21, sawa na Waziri wa Utalii Najib Balala na Waziri Msaidizi wa Ardhi Gideon Mung’aro.

Magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kwale), Amason Kingi (Kilifi), Dhadho Godhana (Tana River), Fahim Twaha (Lamu) na Granton Samboja (Taita Taveta) waliahidi kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Rais Kenyatta.