Uhuru achoshwa na hotuba yake mwenyewe

Uhuru achoshwa na hotuba yake mwenyewe

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumanne bungeni alilalamika kuwa Hotuba yake Kuhusu Hali ya Taifa ilikuwa ndefu na ya kuchosha.

Hii ni licha ya hatua yake ya kujaribu kutosoma matini mengine ya hotuba yake iliyomchukua saa mbili na dakika nane kukamilisha.

“Jamani, nimejaribu kukata lakini ni ndefu sana; hata mimi nimechoka,” Rais Kenyatta akasema huku wabunge na maseneta wakiangua kicheko.

Kiongozi wa taifa alisoma hotuba hiyo akiwa amesimama ndani ya ukumbi wa bunge huku akinywa maji kila mara baada ya kuishiwa na mate.

Muda mfupi baada ya Rais Kenyatta kukamilisha hotuba yake Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchuma Murkomen aliweka ujumbe katika akaunti yake ya twitter akilalamikia urefu wa hotuba hiyo.

“Bunge linafaa kupitisha sheria ya kuweka muda maalum ambao marais watatumia kuwasilisha hotuba zao kuhusu Hali ya Taifa miaka ijayo. Alivyosema aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill, “hotuba nzuri inafaa kuwa fupi kama sketi ya mwanamke,” Bw Murkomen akaandika.

Naye Seneta wa Nakuru Susan Kihika akasema: “Kwa wale ambao wangali wanafuatilia hotuba hiyo ndefu ambayo haina mnato, je, ametoa maelezo kuhusu ufichuzi wa nyaraka za Pandora?”

Kauli sawa na hiyo ilitolewa na mwenzake wa Nandi Samson Cherargei ambaye alifananisha hotuba hiyo na ngano isiyo na maana yoyote kwa Wakenya.

“Hotuba hii haijagusia changamoto ambazo zinawaathiri Wakenya kama vile kupanda kwa gharama ya maisha,” akasema.  

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Saratani ya mifupa inayolemaza waathiriwa

Mafuriko yashuhudiwa mjini Thika

T L