Uhuru adokeza kuwa huenda akaondoa kafyu

Uhuru adokeza kuwa huenda akaondoa kafyu

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amedokeza kuwa huenda akaondoa kafyu hivi karibuni.

Kiongozi wa taifa ambaye alikuwa akiwatuhubia wananchi Jumatatu mjini Karatina alisema kuwa amesikiliza malalamishi ya raia kuhusu suala hilo.

“Katika siku zijazo tutaliangalia suala hilo. Nafanya kazi na hivi karibuni nitatoa taarifa kuhusu kafyu. Hata hivyo, sitaki kuongea mapema,” Rais Kenyatta akawaambia wananchi.

Rais Kenyatta pia aliwataka wakazi kuendelea kuzingatia kanuni zilizotolewa na Wizara ya Afya kuzuia maambukizi ya Covid-19 ili kujikinga na ugonjwa huo ambao umeua mamilioni ya watu duniani na kuvuruga chumi.

“Mnahitaji kujikinga dhidi ya ugonjwa huo ili tutakapofungua hakutakuwa na maafa zaidi. Mtakuwa huru kuishi mtakavyo,” akaongeza.

Rais Kenyatta amesema hayo siku chache baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na yule wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na wafuasi wa Naibu Rais William Ruto kumshinikiza afungue uchumi.

Wanasiasa hao walisema kuwa raia wanapitia ugumu wa maisha na changamoto ambazo zimesababishwa ukame ambao umevuruga maisha ya mamilioni ya Wakenya.

Kando na hao chama cha wamiliki wa mabaa na vilabu vya burudani na wamiliki wa magari ya uchukuzi wa abiria wamemtaka Rais Kenyatta kuondoa kafyu ili waweze kuendesha biashara zao nyakati za usiku.

You can share this post!

Vijana wakaidi wazee 2022

Juventus yaadhibu AS Roma ya kocha Jose Mourinho kwenye...

F M