Habari

Uhuru aelezea matumaini ya BBI 'kusuluhisha changamoto zote nchini'

November 26th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta amesema utaratibu wa kubadilisha katiba kupitia mpango wa BBI utasaidia kusuluhisha changamoto zilizojikita mno nchini kama vile msururu wa vurugu baada ya uchaguzi.

Rais alisema mchakato huo unanuiwa kuimarisha mfumo wa kikatiba wa Kenya kwa kurekebisha sehemu chache zilizoleta utata katika Katiba ya sasa

“Tunahitaji kuimarisha katiba ya 2010 iwapo tutaendelea na safari yetu ya miongo mingi ya kutafuta maslahi bora ya Wakenya,” akasema Rais Kenyatta alipohutubu katika jumba la KICC, Nairobi wakati wa uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji sahihi za marekebisho ya katiba kuambatana na mapendekezo ya BBI.

Alikuwa ameandamana na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Rais Kenyatta alisema hayo Jumatano katika Jumba la KICC katika Kaunti ya Nairobi ambako yeye na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walizindua mchakato wa kutia saini ili kuunga mkono marekebisho ya katiba kuambatana na mpango wa BBI.

“Tunapoanza shughuli za kutia saini, tunatambua kwamba juhudi hizi zinalenga kuhimiza mashauriano ya kidemokrasia kulingana na katiba,” akasema.

Alisema kwamba haja ya kurekebisha katiba ni dhahiri kutokana na tisho lisiloisha la vurugu baada ya uchaguzi na wasiwasi wa umma kuhusu ukosefu wa ushirikishwaji wa wote katika shughuli za serikali.

“Ukweli ni kwamba kimsingi, maisha huhitaji mabadiliko ya mara kwa mara iwapo tutatatua changamoto zetu na kutumia kikamilifu nafasi zilizoko,” akasema Rais Kenyatta akitahadharisha kwamba misimamo mikali ya katiba ni kichocheo cha vita.

Akiangazia baadhi ya mapendekezo bora katika mswada wa BBI, Rais Kenyatta alisema marekebisho hayo yatahakikisha kushiriki kikamilifu kwa wanawake katika ustawi wa kitaifa kwa kuongeza idadi yao katika taasisi za uwakilishi ikiwemo Seneti ambako watachukua asilimia 50 ya viti.

“Hii inamaanisha watasimamia jinsi tutakavyotumia asilimia 35 ya fedha ambazo zitagatuliwa katika maeneo ya kaunti,” akaeleza.

Aidha, Rais Kenyatta alisema kuna mpango mpya wa kuhakikisha uwakilishi zaidi na kamilifu wa wanawake katika Bunge la Kitaifa.

Rais Kenyatta alisema matakwa ya watu wanaoishi na ulemavu pamoja na vijana yameshughulikiwa pia kwenye marekebisho yaliyopendekezwa kwa kuhakikisha kwamba watawakilishwa kikamilifu katika bunge la kitaifa.

Makundi haya mawili yametengewa nafasi sita za uteuzi, nne za wanaoishi na ulemavu na viti viwili vya vijana.

Ili kuhakikisha kila Mkenya anafurahia demokrasia ambayo katiba ya mwaka 2010 iliahidi, Rais alisema mswada wa BBI utasuluhisha tatizo la uwakilishi usiotosha katika baadhi ya maeneo ya nchi.

“Hii itawezesha kuwepo kwa utaratibu wa haki na usawa katika ugavi wa rasilimali za kitaifa,” akasema Rais Kenyatta.

Alisema mapendekezo ya BBI yatahakikisha kushirikishwa zaidi kwa umma katika viwango vyote uwakilishi kama, yaani, wadi, maeneo bunge, serikali ya kaunti na ile ya kitaifa,”

Kiongozi wa Taifa pia alizungumza kuhusu manufaa ya yeye ‘kushirikiana’ na Bw Odinga, akisema hatua hiyo ilituliza taifa na kutoa nafasi ya kutambua marekebisho muhimu ambayo yataimarisha umoja, kushiriki kwa wote, usawa na maongozi bora.

Kwa upande wake, Bw Odinga aliwahimiza Wakenya kujitokeza kwa wingi na kutia saini mswada huo wa BBI kwa muda mfupi ili mchakato huo uingie katika hatua nyingine ya kuelekea kura ya maamuzi.

“Ni wakati muhimu kuwa nchini Kenya na kushiriki katika harakati za kuandika historia. Katika hatua hizi, tunashughulikia matumaini yetu wala sio hofu katika kutafuta umoja na maendeleo tunayoazimia.

“Kwa kutia saini zetu hii leo baada ya kusoma mswada huo, mwaweka alama ya kuidhinisha mchakato huo,” akasema Bw Odinga.

Miongoni mwa viongozi wa vyama waliotia saini stakabadhi hiyo ya BBI kwenye uzinduzi huo walikuwa Musalia Mudavadi (Amani National Congress-ANC), Isaac Rutto (Chama Cha Mashinani-CCM), Wafula Wamunyinyi wa Ford Kenya, Alfred Mutua wa Maendeleo Chap Chap-MCC, Gideon Moi (Kanu) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya.