Habari Mseto

Uhuru aendeleza imani yake kwa jeshi

December 17th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

IMANI ya Rais Uhuru Kenyatta kwa wanajeshi kusimamia idara muhimu serikalini iliendelea kudhihirika jana, baada yake kuzindua Idara ya Kitaifa ya Kusimamia Huduma za Ndege (NASD).

Idara hiyo, ambayo itaongozwa na Wizara ya Ulinzi, itakuwa ikisimamia huduma za ndege katika mashirika yote ya serikali yanayotumia ndege katika uendeshaji wa shughuli zao.

Idara hiyo itasimamia huduma za polisi, Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS), Shirika la Kusimamia Usambazaji wa Huduma za Umeme (Ketraco) na Shirika la Kusimamia Misitu (KFS).

Akihutubu kwenye uzinduzi wa idara hiyo jijini Nairobi, Alhamisi, Rais Kenyatta alisema serikali ilichukua hatua hiyo ili kulainisha huduma za ndege katika mashirika yake.

Alisifu wanajeshi kuhusu vile wamekuwa wakiendesha huduma zao za ndege, akisema tajriba yao itakuwa muhimu kwenye usimamizi wa idara hiyo mpya.

Hatua hiyo inaendelea kudhihirisha imani ya Rais Kenyatta kwa wanajeshi katika usimamizi wa sekta na mashirika muhimu ya serikali tangu aanze kuhudumu katika muhula wa pili mnamo 2017.

Miongoni mwa taasisi muhimu ambazo ameziweka chini ya usimamizi wa jeshi ni Kaunti ya Nairobi, Shirika la Nyama (KMC), Mamlaka ya Kusimamia Huduma za Bandari (KPA), Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kati ya taasisi zingine.

Katika Kaunti ya Nairobi, Rais Kenyatta alimpokonya Gavana Mike Sonko baadhi ya majukumu ya kuliendesha jiji na kumkabidhi Meja Jenerali Mohamed Badi, chini ya Halmashauri ya Kusimamia Jiji la Nairobi (NMS).

Mwezi Septemba, Rais alimwagiza Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya kuanza mchakato wa kuweka KMC chini ya usimamizi wa wanajeshi.

Alisema hilo litalisaidia shirika hilo kuanza kupata faida, hasa kwa wafugaji.

Licha ya kukosolewa na baadhi ya Wakenya kuhusu mbinu hiyo, Rais Kenyatta amejitetea akilisifia jeshi kwa kuonyesha nidhamu kubwa katika uendeshaji wa taasisi hizo.