Habari

Uhuru aepuka siasa ziarani Eldoret

June 21st, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, Ijumaa waliepuka siasa walipozindua kiwanda cha nguo cha Rivatex, Kaunti ya Uasin Gishu.

Japo ilitarajiwa kuwa joto la siasa lingepanda katika ziara ya Rais eneo hilo, viongozi waliepuka siasa na kuzungumzia masuala ya kujenga taifa.

Rais Kenyatta aliongoza kwa kuzungumzia masuala ya maendeleo na kujenga uchumi, akisema hayo ndiyo ya manufaa kwa Wakenya, badala ya kuendeleza ukabila ama siasa duni.

“Na mambo haya ndiyo sisi twahitaji. Sisi hakuna lingine lolote ambalo tunatafuta, ni kuhakikisha ya kuwa tumefanya kazi na kuinua na kubadilisha maisha ya Wakenya wote,” akasema Rais Kenyatta.

Rais aliahidi kuwa serikali itafufua viwanda vyote ambavyo vilikuwa vimekufa, ili visaidie jamii na kuzidisha nafasi za ajira kwa Wakenya.

“Mwishowe kila kijana hapa, awe ni Mkalenjin, Mkikuyu, Mjaluo, Mkamba au Mgiriama apate kazi ili aweze kuwa na pesa zake za mfuko,” Rais akaongeza.

Naibu wake, aidha aliepuka siasa katika hotuba yake, mara kwa mara akimmiminia sifa Rais kuhusu miradi ya maendeleo ambayo serikali imetelekeza kama ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ya humu nchini.

Ucheshi

Mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, ambaye alizungumza kama kiongozi wa eneo hilo alizua ucheshi, tofauti na siasa zake kali kila anapomtetea Naibu Rais, Dkt Ruto.

“Haya sasa ndiyo matunda ya Nguzo Nne Kuu na ya Jubilee,” alisema Bw Sudi.

Bw Sudi na Gavana wa Uasin Gishu, Bw Jackson Mandago ambao ni wafuasi sugu wa Naibu Rais walitumia hotuba zao kumfurahisha Rais na kuepuka matamshi makali ambayo yamekuwa yakitawala mikutano ya kisiasa siku za hivi majuzi.

“Ulipotuacha tulipokupigia kura bado tuko hapo. Na wewe ujue wewe ni mzigo wetu na sisi ni mzigo wako, hakuna kupiga kona. Ukiwa hapa uko nyumbani kuliko pengine popote,” alisema Bw Sudi.