Uhuru afunga kaunti 5

Uhuru afunga kaunti 5

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA zaidi ya milioni 12 wa kaunti za Nairobi, Kiambu, Kajiado, Machakos na Nakuru wamepunguziwa uhuru wa kusafiri, kutangamana, kustarehe na kufanya kazi kwa muda usiojulikana.

Hii ni baada ya serikali kutangaza marufuku ya kutoka au kuingia katika kaunti hizo zenye jumla ya wakazi milioni 12, kutokana na kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya virusi vya corona.

Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kaunti hizo kuwa maeneo hatari na kuzifunga kwa muda usiojulikana kuanzia leo.

Wakazi wa kaunti hiyo hawataweza kutoka nje au wa kaunti zingine kuingia humo hadi serikali itakapoondoa marufuku hiyo.

“Safari zote za barabarani, reli, na ndege kuingia na kutoka kaunti za Nairobi, Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru zimesitishwa kuanzia usiku wa manane leo,” akatangaza Rais akihutubia taifa Ijumaa.

Alisema hatua hii imechukuliwa baada ya kubainika kwamba asilimia 70 ya maambukizi ya virusi vya corona yameripotiwa katika kaunti hizo tano.

Marufuku hiyo ni pigo kwa watu waliopanga kutembelea maeneo ya mashambani msimu wa sherehe za Pasaka. Kwa kawaida, watu hutembelea jamaa zao na kuzuru maeneo ya burudani hasa katika miji ya Mombasa, jambo ambalo hawataweza mwaka huu.

Rais Kenyatta pia aliongeza muda wa marufuku ya kutotoka nje usiku katika kaunti hizo kutoka saa nne usiku hadi saa mbili usiku, na akafunga baa na maeneo ya ibada kwa muda usiojulikana. Hii ni pigo kwa Wakristo ambao msimu wa Pasaka huwa ni muhimu kwa imani yao.

Katika maeneo hayo mikahawa itafungwa isipokuwa kwa wateja wanaonunua na kuondoka.

Wakazi wa kaunti nyingine wataendelea kuzingatia kanuni za awali za kuzuia maambukizi ya corona isipokuwa hawataweza kuingia kaunti hizo tano.

Rais Kenyatta pia alipunguza idadi ya watu wanaofaa kuhudhuria sherehe za harusi hadi 30. Watakaohudhuria mazishi hawafai kuzidi 15 na wadumishe kanuni zote za Wizara ya Afya. Mili yote inafaa kuzikwa ndani ya saa 72.

Rais pia alifunga taasisi zote za masomo kwa muda usiojulikana isipokuwa wanafunzi wanaofanya mitihani, na wanasomea uuguzi, matibabu na madaktari.

Shughuli zote za michezo pia zimepigwa marufuku vikiwemo vilabu vya kibinafsi ambako wanachama hukutania.

Rais Kenyatta alisema hatua hizo kali zimechukuliwa baada ya wataalamu kuonya kuwa kuna hatari ya kuongezeka kwa maambukizi ya corona katika kaunti hizo.

“Huduma za baa zimesitishwa katika kaunti za Nairobi, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nakuru. Uuuzaji wa pombe katika mikahawa na mahoteli umepigwa marufuku hadi itakapoagizwa viginevyo,” aliagiza Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta aliagiza waajiri wote wakiwemo wa serikali na kibinafsi kuruhusu wafanyakazi kuhudumu kutoka nyumbani, isipokuwa wale wanaotoa huduma muhimu zizowezekana wakiwa nyumbani.

Kufuatia ongezeko miongoni mwa viongozi na maafisa wakuu wa serikali, Rais Kenyatta alisitisha mikutano ya Baraza la Wawaziri na kamati zake zote kwa muda usiojulikana, vikao vya bunge la kitaifa na mabunge ya kaunti za Nairobi, Machakos na akaagiza mahakama na idara zote katika mfumo wa haki kuchukua hatua za kuzuia maambukizi.

“Kwa makubaliano na uongozi wa mabunge yote mawili na uongozi wa kaunti, vikao vya bunge vikiwemo vya kamati mbali mbali za mabunge ya kaunti za Nairobi, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nakuru, vimesimamishwa hadi itapotangazwa tena,” alisema.

Wageni na Wakenya wanaotoka mataifa ya nje hawataruhusiwa kusafiri nje ya kaunti hizo hadi marufuku hiyo itakapoondolewa.

Nazo hospitali zote nchini zimeagizwa kuruhusu watu wawili pekee katika wodi kutembelea wagonjwa waliolazwa.

Alisema kwamba kiwango cha maambukizi katika kaunti hizo tano kimeongezeka na kufikia hali ya kutisha.

Kaunti ya Nairobi ina asilimia 60 ya maambukizi yote nchini. Hii inamaanisha kuwa kwa kila watu 10, sita wameambukizwa corona.

Alisema kwamba katika kipindi cha siku 13 pekee, idadi ya wagonjwa wa corona wanaolazwa hospitalini imeongezeka kwa asilimia 52.

“Wataalamu wetu wa afya wanaonya kwamba wimbi la tatu lilianza kupata nguvu mwanzo wa Machi 2021. Wimbi hilo linatarajiwa kushika kasi katika muda wa siku 30 zijazo ambapo visa 2,500 na 3,000 vitakuwa vikiripotiwa kwa siku,” alisema.

Aliongeza kuwa wimbi hili litapungua kati kati ya Mei mwaka huu, siku 60 kutoka Ijumaa.

You can share this post!

Wabunge kukutana Jumanne kuahirisha vikao vya ana kwa ana

Kang’ata sasa akiri ameonja makali ya Covid-19 mara...