UHURU AFYEKEA RAILA NJIA

UHURU AFYEKEA RAILA NJIA

Na BENSON MATHEKA

HUKU uchaguzi mkuu wa 2022 ukiendelea kukaribia, Rais Uhuru Kenyatta anaonekana kuchukua hatua za wazi na zinazoonekana kumwandalia kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, njia ya kuingia ikulu.

Hatua ya chama cha Jubilee kusuka muungano na chama cha ODM cha Bw Odinga na kugawanyika kwa eneo la Mlima Kenya, zinachukuliwa kama mojawapo ya mbinu za Rais Kenyatta kuhakikisha kuwa waziri mkuu huyo wa zamani atakuwa rais wa tano wa Kenya.

Viongozi wanaosuka muungano huo wanasema kwamba, wana maagizo kutoka kwa viongozi wa vyama vyao kuufanikisha bila kuhusisha vyama vingine kwanza, kama hatua ya kuendeleza handisheki waliyoanzisha wao wawili.

“Tumepatiwa maagizo ya kuhalalisha muungano wa vyama vyetu vya Jubilee na ODM. Wanasiasa wa vyama vingine wanaweza kuungana nasi baadaye bila masharti,” alisema Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju.

Ingawa Bw Odinga anasisitiza kwamba hajatangaza azima yake ya kugombea urais, kuna kila ishara katika matamshi na hatua za Rais Kenyatta kuwa anamtengenezea njia kwa kumuondolea vizingiti vinavyoweza kumzuia kumrithi ikulu.

Hatua ya kwanza ya kufanya hivyo ilikuwa ni kumtema naibu wake William Ruto ambaye kulingana na wadadisi wa siasa, ndiye mpinzani mkuu wa Bw Odinga.

“Rais Kenyatta aligawanya chama tawala cha Jubilee, hatua iliyonuiwa kumnyima Dkt Ruto fursa ya kutumia chama hicho kilicho na uwezo na maarufu kote nchini kumtatiza Bw Odinga katika safari yake ya kuingia ikulu,” asema mbunge wa Soy Caleb Kositany.

Ingawa walipounganisha vyama vyao vya The National Alliance (TNA) na United Republican Party (URP) kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017 walisema kwamba, walilenga kumtengenezea Dkt Ruto chombo cha kuingia ikulu baada ya Rais Kenyatta kutawala kwa mihula miwili, kiongozi wa nchi alibadilisha nia na kusema sio lazima Kenya iongozwe na makabila mawili.

Marais wanne tangu uhuru wametoka jamii za Agikuyu(3) na Kalenjin(1).

“Hata mimi ninaweza kusema wakati wa rais kutoka makabila mengine umefika,” Rais Kenyatta alisema alipohudhuria mazishi ya mamake kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi mwaka jana.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakiendeleza mchakato wa kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao walilenga kutumia kuunganisha wanasiasa wakuu kusimama nyuma ya Bw Odinga.

Rais Kenyatta amekuwa akitofautiana na wanasiasa wa Mlima Kenya wanaomuunga Dkt Ruto akiwemo seneta wa Murang’a, Irungu Kang’ata aliyemweleza kwamba, BBI sio maarufu katika Mlima Kenya.

Akizungumza Kisumu siku ya Madaraka mwaka huu, Rais Kenyatta alitoa ishara kwamba chaguo la mrithi wake ni Bw Odinga kwa kutangaza kwamba wataendelea kushirikiana siku zijazo.

“Nitaendelea kushirikiana na ndugu yangu, Jakom, Raila Odinga siku zijazo kwa kuwa alinishika mkono bila masharti yote,” Rais Kenyatta alisema.

Hatua iliyoshangaza wengi baada ya kauli hiyo ni kutawazwa kwa Spika wa Bunge Justin Muturi kuwa msemaji wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya ambayo imeligawanya kisiasa.

Wadadisi wanasema hii ni mbinu ya kupunguza umaarufu wa Dkt Ruto ambao umekataa kudidimia eneo hilo licha ya kutengwa serikalini.

Rais Kenyatta pia amenukuliwa akiwataka vinara wa uliokuwa muungano wa NASA kuungana katika safari ya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 na akaashiria kwamba atamuunga mmoja wao kuwa mrithi wake.

Vinara wawili wenza wa muungano huo Musalia Mudavadi wa ANC, Kalonzo Musyoka wa Wiper wametangaza kuwa majina yao yatakuwa kwenye debe na kamwe hawatamuunga Bw Odinga.

Wadadisi ambao hawakutaka tuwataje majina walisema wawili hao waligundua kwamba Rais Kenyatta ameamua kumuunga Bw Odinga kwa kuwataka kuvunja muungano wao wa One Kenya Alliance unaohusisha Moses Wetangula wa Ford Kenya na Gideon Moi wa Kanu.

Inasemekana OKA ulikuwa wazo la baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya ambao walitaka kumzuia Bw Odinga kupata baraka za Rais Kenyatta lakini hawakuweza kumshawishi kiongozi wa nchi.

OKA ulitikiswa Bw Moi ambaye amekuwa mshirika wa Rais Kenyatta kumkumbatia Bw Odinga na kumtembelea nyumbani kwake Nairobi na Kisumu.

Duru zinasema juhudi zinaendelea kuwashinikiza vinara wa OKA kumuunga Bw Odinga kwa msingi kwamba Dkt Ruto akishinda hataweza kuaminika kulinda maslahi yao.

Mbunge mmoja wa chama cha Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake alisema kwamba, vinara wa OKA wanataka hakikisho kuwa maslahi yao yatazingatiwa. “Rais Kenyatta atakuwa mdhamini wa hakikisho hilo kwa kuwa hataki Dkt Ruto kuingia Ikulu,” alisema.

You can share this post!

Colombia na Venezuela waambulia sare tasa kwenye Copa...

Kashfa ya vyama kadha kusajili raia kwa lazima yakera...