Habari

Uhuru agutuka nyumbani kukavu

July 1st, 2020 2 min read

KENNEDY KIMANTHI na DAVID MUCHUI

RAIS Uhuru Kenyatta ameanza kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika ngome yake ya kisiasa eneo la Kati, baada ya kuwapuuza kwa muda mrefu viongozi waliokuwa wakimkashifu kwa kutelekeza eneo hilo kimaendeleo.

Hayo yamedhihirika wakati huu Rais anapanga kuzuru eneo hilo ilhali bado hakuna miradi muhimu ambayo anaweza kuzindua.

Kutokana na haya, Rais Kenyatta ametuma mawaziri wake kwa wiki tatu sasa kuzuru maeneo ya Mlima Kenya kukagua na kuweka mikakati ya kuharakisha miradi.

Kwa kipindi kirefu tangu Rais alipoweka mkataba wa maelewano na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya wamekuwa wakimkashifu kwa kupeleka maendeleo katika ngome za kiongozi huyo wa upinzani ilhali ngome yake imesalia nyuma.

Wakosoaji wake ambao ni wandani wa Naibu Rais William Ruto, walikuwa wakirejelea miradi mikuu ambayo Rais huanzisha katika maeneo kama vile Nyanza na Mombasa ambako kuna ufuasi mkubwa wa Bw Odinga.

Katika wiki chache zilizopita, baadhi ya mawaziri ambao wamekita kambi Mlima Kenya ni Fred Matiang’i (Usalama wa Nchi), James Macharia (Uchukuzi), Amina Mohamed (Michezo), Najib Balala (Utalii), Mutahi Kagwe (Afya), Peter Munya (Kilimo) na Waziri Msaidizi wa Biashara Lawrence Karanja.

“Lazima tuhakikishe kuna miradi ambayo Rais anaweza kujionea atakapokuja. Tumekagua miradi yote na kukubaliana kwamba miradi inayokumbwa na changamoto ni barabara kwa hivyo wakandarasi wataagizwa watie bidii,” alisema Gavana wa Meru, Bw Kiraitu Murungi baada ya kukutana na Dkt Matiang’i.

Dkt Matiang’i husimamia kamati ya baraza la mawaziri ambapo anakagua utekelezaji wa mipango ya serikali kupitia wizara zote, kando na wadhifa wake wa uwaziri.

Inaaminka Rais amepanga kuzuru eneo la Mlima Kenya mnamo Agosti.

Rais amekuwa akipuuzilia mbali wakosoaji wake wanaodai ametelekeza Mlima Kenya licha ya kuwa na ufuasi mkubwa, akisema yeye ni kiongozi wa taifa lote.

Wakosoaji hao katika mrengo wa ‘Tangatanga’ hutaja miradi mikubwa ya maendeleo inayopewa kipaumbele katika maeneo yaliyokuwa ngome za upinzani katika chaguzi zilizopita kama vile ukarabati wa bandari ya Kisumu na miundomsingi mbalimbali Pwani.

Miongoni mwa miradi mikubwa ambayo haijakamilika eneo la Kati ni barabara ya Mau Mau ambayo itaunganisha Kaunti za Nyeri, Kiambu, Murang’a na Nyandarua. Barabara hiyo ya kilomita 540 itagharimu serikali Sh30 bilioni.

Ujenzi wa barabara muhimu ya Kenol-Sagana-Maua pia haujaanza ingawa Waziri Macharia alisema utaharakishwa.

Mradi ambao umeshika kasi, na huenda ukazinduliwa na Rais, ni ukarabati wa reli ya kutoka Nanyuki hadi Nairobi.

“Tumeahidiwa kuwa ujenzi wa barabara zote utaharakishwa na zile zilizoharibika zitafanyiwa ukarabati,” akasema Mbunge wa Imenti ya Kati, Bw Moses Kirima.

Mwenzake wa Igembe ya Kati, Bw Kubai Iringo alisema mradi mwingine unaotarajiwa kuharakishwa ni ujenzi wa kambi ya kikosi cha polisi wa GSU katika mpaka wa Meru na Isiolo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Michezo aliagiza ujenzi wa uwanja wa michezo wa Kinoru ukamilkike ndani ya siku 20.

Waziri Msaidizi Karanja naye alizindua ujenzi wa kiwanda cha kuhifadhi viazi Meru, akisema kingine kitazinduliwa Nyandarua mwezi Agosti.

Bw Munya pia amefanya ziara nyingi katika Kaunti za Murang’a, Tharaka-Nithi na Meru hasa kuhusu changamoto zinazokumba sekta ya kahawa kwa lengo la kufufua viwanda.