Habari MsetoSiasa

Uhuru ahepa swali la ikiwa anaumezea Uwaziri Mkuu

January 15th, 2020 2 min read

 Na LEONARD ONYANGO

MGAWANYIKO ndani ya chama cha Jubilee huenda ukaendelea baada ya Rais Uhuru Kenyatta jana kukataa kutangaza msimamo ikiwa anamezea mate wadhifa wa Waziri Mkuu au la.

Rais Kenyatta Jumanne alikataa kuzungumzia madai ambayo yamekuwepo kwamba anataka kuwa waziri mkuu baada ya kukamilisha muhula wake wa pili 2022.

“ Haa..hiyo nyinyi ndio mnasema. Mimi nilisema yangu nikamaliza,” Rais Kenyatta akajibu wanahabari alipoulizwa ikiwa anamezea mate wadhifa wa waziri mkuu.

Mjadala kuhusiana na wadhifa wa waziri mkuu umezua joto ndani ya chama cha Jubilee huku wandani wa Naibu wa Rais William Ruto wakisisitiza kuwa hawataruhusu Rais Kenyatta kusalia mamlakani baada ya 2022.

Wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Dkt Ruto wanasema kuwa lengo kuu la ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI) ni kubuni wadhifa wa waziri mwenye mamlaka ya juu kuliko rais.

Wanasiasa wa kundi la Tangatanga wanahisi kuwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka huenda ukamkosesha Dkt Ruto kiti cha urais 2022.

Wiki iliyopita, Dkt Ruto alisema: “Najua Rais Kenyatta ni muungwana na mpenda demokrasia hana mpango wa kukatalia mamlakani baada ya 2022.”

Jana, Rais Kenyatta alitofautiana na Dkt Ruto kwamba ripoti ya BBI imesababisha mgawanyiko zaidi nchini.

“Sioni kwamba kuna mgawanyiko nchini. Niliweka wazi tangu mwanzoni mwa muhula wangu wa pili kwamba lengo langu kuu ni kuunganisha Wakenya,” akasema Rais Kenyatta.

“Inasikitisha kwamba katika harakati za kuunganisha Wakenya baadhi ya watu wanadhani kwamba wameachwa nyuma,” akaongezea.

Kiongozi wa nchi aliwataka wanasiasa kutumia mjadala kuhusu BBI kutangamana badala ya kurushiana cheche za maneno.

“Tusiruhusu siasa za mashindano kutuzuia kushughulikia masuala muhimu yanayowahusu Wakenya. Lengo kuu la BBI si kuwatengenezea watu nyadhifa bali ni kuboresha utawala.

“BBI inatupa fursa ya kujadili namna ya kukabiliana na ufisadi humu nchini na kuwatafutia vijana nafasi za ajira. Wakenya wanahitaji ustawi wa kiuchumi bali si mashindano ya kiuchumi,” akasema.

Aliwataka viongozi wa kisiasa kushirikiana kwa ajili ya ustawi wa nchi hii badala ya kuzozana katika majukwa ya kisiasa.