Michezo

Uhuru ahimiza uwajibikaji zaidi katika usimamizi wa viwanja Kenya

September 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

RAIS Uhuru Kenyatta amewaonya vikali vinara wa Sports Kenya na kuwataka kuhakikisha kwamba viwanja vinavyojengwa na kukarabatiwa na serikali vinasimamiwa kwa njia inayofaa.

Akifungua upya uwanja wa Nyayo jijini Nairobi hapo Jumamosi, Rais aliitaka pia Sports Kenya na Wizara ya Michezo kuhakikisha kuwa shughuli zote zinazoendelea za ujenzi na ukarabati wa viwanja vya humu nchini zinakamilika rasmi kufikia Disemba mwaka huu.

“Lazima viwanja hivi visimamiwe vyema na vifaa vilivyomo kuwekwa chini ya uangalizi bora ili kupunguza gharama kubwa ya ukarabati wa mara kwa mara,” akasema Uhuru.

Miongoni mwa viwanja vinavyokarabatiwa kwa sasa na serikali ni MISC Kasarani jijini Nairobi, Kipchoge Keino mjini Eldoret, Kamariny katika Kaunti ya Elgeyo-Marakwet na Wote katika Kaunti ya Makueni.

Rais pia ameagiza Wizara ya Michezo kushirikiana na maafisa husika kutoka serikali za Kaunti za Mombasa, Kisii, Narok na Nakuru kuhakikisha kwamba viwanja vinavyojengwa na kukarabatiwa katika maeneo hayo vinafikia viwango vinavyotakikana kimataifa.

Rais pia alifichua mipango ya kujengea Jeshi la Kenya (KDF) uwanja wa kisasa wa michezo katika Kambi ya Lang’ata, Nairobi.

Ameshikilia kwamba kufunguliwa upya kwa uwanja wa Nyayo uliojengwa na kuzinduliwa mnamo 1983, ni mwanzo mpya katika historia ya maendeleo ya michezo nchini Kenya.

“Wanaspoti wetu sasa watakuwa na kila sababu ya kuthibitishia dunia kwamba Kenya ndiyo ngome ya michezo.”

Rais amesema serikali yake itahakikisha kwamba mashindano ya Riadha za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 na Safari Rally yanaandaliwa humu nchini kwa mafanikio makubwa mwaka ujao licha ya changamoto tele ambazo zimechangiwa na janga la corona kwenye ulingo wa michezo.

Uhuru ameitaka pia Wizara ya Michezo kujitahidi maradufu na kuhakikisha kwamba shughuli za spoti zinarejelewa haraka iwezekanavyo.

“Baadhi ya michezo imerejelewa, lakini nahimiza Wizara ya Michezo ifanye juu chini kuona kwamba fani nyinginezo zinafunguliwa,” akasema Uhuru kwa kutaka maandalizi kwa minajili ya Olimpiki zijazo za Tokyo, Japan kushika kasi.

Kati ya watu mashuhuri walioandamana na Uhuru uwanjani Nyayo ni Waziri wa Michezo Amina Mohamed, Gavana wa Kaunti ya Nairobi Mike Sonko, Katibu wa Wizara ya Michezo Joe Okudo, Naibu Waziri wa Michezo Hassan Noor, Mwenyekiti wa Sports Kenya Fred Muteti, na Mwenyekiti wa Hazina ya Michezo, Jack Tuwei.

Miaka mitatu

Uwanja wa Nyayo ambao una uwezo wa kubeba mashabiki 30,000, ulifungwa mnamo 2017 ili ufanyiwe ukarabati kabla ya kuandaliwa kwa mashindano ya soka ya wachezaji wanaocheza barani Afrika katika mataifa yao (CHAN).

Kenya ilifaa kuandaa kipute cha CHAN 2018, lakini ikapokonywa idhini na kivumbi hicho kuhamishiwa Morocco baada ya viwanja kukosekana.

Uga wa Nyayo uliwahi kufunguliwa Agosti 2017 kwa debi ya Mashemeji kati ya Gor Mahia na AFC Leopards na kufungwa tena kwa ajili ya ukarabati. Uwanja huu, ambao ulitumiwa kwa mechi nyingi za Ligi Kuu ya Soka Kenya (KPL) kabla ya 2017, ulifunguliwa tena kidogo kwa mbio za Beyond Zero mnamo Machi 8 baada ya kutumiwa kuombolezea rais wa pili wa Kenya, Daniel arap Moi mnamo Februari 11, 2020.

Shughuli ya kwanza ya kimichezo iliyoandaliwa ugani Nyayo ni mjarabu wa mbio za kupima utayari wa Kenya kuandaa duru ya mwisho ya mbio za dunia za mabara almaarufu World Continental Tour.

Rais alitumia vifaa vipya vya riadha kuanzisha mbio za mita 400 kwa upande wa wanawake na wanaume katika mjarabu huo ulioshirikisha wamtimkaji 54 katika vitengo vya mita 200, mita 400 na mita 800 kwa upande wa wanaume na wanawake, mita 4×400 kupokezana vijiti (wanawake kwa wanaume) na urukaji mbali (wanawake).

Washiriki wa mita 400 zilizoanzishwa na Rais Kenyatta ni:

Wanawake: Linda Kageha (Nyanza South), Gladys Musyoki (Police), Maureen Thomas (Nyanza South), Everngeline Makena (Eastern), Tabitha Mogina (KDF), Elizabeth Katugwa (Police), Jacinta Shikanda (Police), Veronica Mutua (Police).

Wanaume: Joseph Poghisio (KDF), William Rayian (Police), Jared Momanyi (KDF), Stanley Kieti (Police), Emmanuel Mutua (Southern), David Sanayek (Prisons), Joseph Sanare (KWS), Benson Lekishon (Eastern).