Michezo

Uhuru aipokeza Harambee Stars bendera ya taifa

May 31st, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

RAIS Uhuru Kenyatta amewasihi wachezaji wa Harambee Stars wajiamini na kucheza kwa kujituma watakapokuwa nchini Misri kushiriki fainali za Mataifa Bingwa barani Afrika (Afcon).

Rais alitoa ushauri huo Alhamisi alipoipa timu hiyo bendera ya taifa na kuiaga rasmi kushiriki fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Akiwakabidhi bendera hiyo kwenye halfa iliyofanyika katika Ikulu, Rais aliwataka wachezaji hao na maafisa wao wa kiufundi wawe mabalozi wema hata kama hawatafanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

“Si lazima mshinde ubingwa. Muhimu zaidi ni kupeperusha bendera ya taifa na kutuwakilisha vyema kimataifa,” alisema.

Timu hiyo iliondoka nchini Alhamisi usiku kupiga kambi eneo la Marcoussis, Kusini mwa Paris kabla ya kuelekea nchini Misri baada ya kushiriki mechi mbili za kipimana nguvu dhidi ya Madagascar na DRC Congo.

Hii ni mara ya 15 kwa Harambee Stars kushiriki katika mashindano haya ya bara baada ya kipindi cha miaka 15. Mara ya mwisho ilikuwa 2004 dimba hilo lilipofanyika nchini Tunisia.

Kocha wa Harambee Stars, Sebastian Migne alimshukuru Rais kwa kuhakikisha timu imepata usaidizi wa kutosha kutoka kwa Hazina ya Kitaifa ya Michezo (NSF).

“Tumejiandaa vyema kuwakilisha taifa ipasavyo nchini Misri. Asante sana kwa kutuunga mkono,” alisema kocha huyo atakayeongoza kikosi cha wachezaji 27 kwa ajili ya michuano hiyo ya Afcon.

Wengine kuingia kambini baadaye

Wachezaji 14 tayari wako barani Ulaya ambapo wamefanyiwa mipango ya kujiunga na wenzao kambini baada ya kuhudumia klabu zao barani humo.

Rais Kenyatta alihakikishia timu hiyo uungwaji mkono hadi itakaporejea nchini baada ya kumalizika kwa fainali hizo.

“Kila safari huanza kwa hatua. Hazina ya Kitaifa ya Michezo itahakikisha timu zote za taifa zinapewa ufadhili wa kutosha,” alisema Rais.

Stars itacheza mechi yake ya kwanza mnamo Juni 23 dhidi ya Algeria kabla ya kuvaana na majirani Tanzania hapo Juni 27 kabla ya kukabiliana na Senegal mnamo Julai Mosi.

Katika mechi za mchujo, Harambee Stars ilikuwa katika Kundi C pamoja na Sierra Leone, Ghana na Ethiopia ambapo ilimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Ghana.

Waziri wa Michezo na Turadhi za Kitaifa, Amina Mohamed aliyeandamana na timu hiyo kwa hafla hiyo alisema wizara yake ilitoa Sh244 milioni kwa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) kusaidia timu hiyo katika maandalizi ya michuano ya Afcon.