Habari MsetoSiasa

Uhuru akaa ngumu kuhusu marufuku ya kampuni za kamari

August 25th, 2019 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

WARAIBU wa mchezo wa kamari wataendelea kuumia kiuchumi, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kusema kwamba kampuni za michezo ya bahati nasibu lazima zilipe ushuru kabla ya kuruhusiwa kuendelea na biashara zao nchini.

Rais Kenyatta alitetea oparesheni iliyoendeshwa dhidi ya kampuni za kamari majuzi, akisema alishangazwa na jinsi ‘watu’ watano walikuwa wakinufaika na mapato makubwa yaliyotokana na mchezo huo, kinyume cha sheria.

Kiongozi wa nchi aliyatoa matamshi hayo Jumamosi wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Christ Is The Answer Ministries (Citam) eneo la Karen, Nairobi.

Matamshi yake yalitokana na malalamishi ya Askofu wa Kanisa hilo, Dkt David Oginde kwamba serikali inafaa kuzima kamari na maovu mengine kama uavyaji mimba na ushoga, matatizo aliyoyasema yatachangia kusambaratika kwa taifa hili kimaadili.

“Nakubaliana na askofu kwamba kamari ni mchezo mbaya. Ni wajibu wa viongozi wetu kubadilisha sheria na kuzima kamari. Nitaunga sheria hiyo mkono,” akasema Rais Kenyatta.

Rais pia alishikilia kwamba iwapo kamari itaendelea nchini, basi lazima kampuni zinazoshiriki mchezo huo zilipe ushuru liwalo na liwe na pia zifuate sheria za taifa.

“Sheria zipo na pia ushuru upo. Hata Biblia takatifu inasema mpe Mungu kilicho chake na Kaisari kilicho cha Kaisari. Kama Kaisari lazima nipokezwe fungu langu iwapo kamari itaendelea nchini,” akaongeza Rais Kenyatta.

Kiongozi wa nchi alikuwa ameandamana na Naibu Rais Dkt William Ruto, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Waziri wa Utumishi wa Umma, Prof Margaret Kobia, Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi, Esther Passaris miongoni mwa viongozi wengine wakati wa maadhimisho hayo.

Bodi ya Kudhibiti na Kutoa Leseni za Kamari (BLCB) chini ya Dkt Matiang’i iliagiza kampuni za mawasiliano zizime nambari maalum za malipo na za kutuma arafa kwa kampuni 27 za kamari kisha kusitisha shughuli zao nchini.

Hatua hiyo ilifanyika baada ya Dkt Matiang’i kudai kwamba kampuni hizo hazijakuwa zikitii sheria zinazoongoza mchezo huo na pia zimekuwa zikikwepa kulipa ushuru kwa serikali kinyume cha sheria.

Hata hivyo, hatua hiyo ilipingwa na wamiliki wa kampuni hizo, huku hali hiyo ikizamisha ufadhili wa michezo mbalimbali.

Baadhi ya kampuni hizo zilikuwa zikitoa kiasi kikubwa cha pesa kusimamia malipo ya mishahara ya wachezaji wa klabu za soka, raga na hata Ligi ya Soka nchini (KPL).

Aidha, kupitia uwekezaji wao, maelfu ya Wakenya ambao hawakuwa na ajira walikuwa wakijipatia riziki.

Lakini wasiwasi mkubwa kutoka kwa sehemu kubwa ya wananchi ni jinsi ambavyo, michezo hiyo ya bahati nasibu imewafanya vijana wengi kutojishughulisha na kutafuta kazi za kufanya.