Habari

Uhuru alimtuma Kamanda kwa Raila?

September 22nd, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

MAELEZO ya kina yameibuka kuhusu mkutano wa siri kati ya kiongozi wa ODM Raila Odinga na Mbunge Maalum wa Jubilee, Maina Kamanda ambapo walijadili uchaguzi mdogo wa Kibra, huku duru zikisema kikao hicho kiliidhinishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Mkutano huo wa saa mbili katika afisi za Bw Odinga kwenye jumba la Capitol Hill, Nairobi, pia ulizungumzia shughuli za Kamati ya Maridhiano (BBI) iliyoundwa kufuatia handisheki kati ya Rais Kenyatta na kigogo huyo wa upinzani.

Kikao hicho kilifanyika saa chache baada ya Naibu Rais William Ruto na washirika wake wa mrengo wa ‘Tangatanga’ katika chama cha Jubilee, kufika Ikulu ambapo Rais Kenyatta alimuidhinisha mgombea wa Jubilee katika uchaguzi wa Kibra, Bw McDonald Mariga.

Duru zinasema kuwa, kikao cha Capitol Hill kiliidhinishwa na Bw Kenyatta ili kuondoa wingu la tashwishi na usaliti lililokuwa limegubika handisheki baada ya Jubilee kuteua mgombeaji katika ngome ya Bw Odinga.

Alipoulizwa iwapo alitumwa na Rais, Bw Kamanda hakukana wala kuthibitisha.

Alisema: “Msitie shaka, mnajua Rais anathamini handisheki kama tu chama chake. Anaijali kwa kuunganisha nchi. Wala hatuwezi kuruhusu Kibra kuharibu handisheki hiyo. Ajenda yake nambari moja ni handisheki kwa manufaa ya taifa.”

Viongozi hao walijadili jinsi maafisa wa Jubilee, tawi la Nairobi, Baraza la Wazee wa Kikuyu na jamii ya kibiashara jijini watashirikishwa katika juhudi za kuhakikisha kura za jamii ya Agikuyu eneo la Kibra zinamuendea Bw Okoth.

Bw Kamanda amembatiza Bw Okoth “mgombeaji wa handisheki”. Taifa Jumapili imefahamishwa kuwa, mikutano ya kuhamasisha makundi hayo matatu kuhusu mikakati iliyopo, itaanza leo huku Bw Kamanda na baadhi ya wanachama wake wa mrengo wa ‘Kieleweke’ katika Jubilee, wakirai jamii ya Gikuyu kumpa Bw Okoth kura zao.

Vilevile, mikutano ya kuomba kura za jamii hiyo nayo zitaanza kesho Jumatatu Bw Kamanda akisema kuwa, watabisha hodi kwa kila mlango kuhakikisha mgombea huyo wa ODM anashinda kwa kura nyingi mno.

“Tulipanga jinsi tutatekeleza kampeni za Imran Okoth huko Kibra ili ashinde pakubwa. Ilikuwa makosa kwa chama cha Jubilee kumteua mgombea Kibra. Ni kama Bw Odinga asimamishe mgombea Gatundu ambako ni ngome ya Rais.

Mbunge huyo maalum alikejeli uteuzi wa Bw Mariga akishangaa jinsi mtu ambaye hajawahi kupiga kura wala si mwenyeji wa Kibra, anaweza kuungwa mkono na chama cha Jubilee.

Kulazimisha

Alimshutumu Naibu Rais Dkt Ruto kwa kulazimishia wakazi wa Kibra Bw Mariga.

“Unamteua vipi mtu ambaye hajawahi kupiga kura hata Kibra halafu utarajie tumpigie debe. Huyo kijana amelazimishiwa watu wa Kibra na Dkt Ruto. Kulikuwa na wawaniaji wengine thabiti ambao wanaweza kuchaguliwa,” akasema Bw Kamanda.

Aliongeza: “Nia ya Bw Ruto sio kumfanya Bw Mariga ashinde kiti cha Kibra, lengo lake ni kuyumbisha handisheki kwa kuzua tashwishi kati ya wafuasi wa Rais na Bw Odinga. Ndiposa mimi nitaongoza kampeni kuhakikisha Bw Okoth anashinda kwa kivumbi.”

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu alimtaja Bw Mariga kama mgombea wa Tanga Tanga, na kuapa kwamba hatakanyaga Kibra kumpigia debe mgombea huyo wa Jubilee ila tu Rais pia aelekee huko.

“Tunafaa kukumbuka kwamba chama cha Jubilee, ingawa kina mirengo miwili, kiko na kiongozi mmoja ambaye ni Bw Kenyatta. Mgombea wa ‘Tangatanga’ ndiye aliidhinishwa na kiongozi wa chama ndio maana ni viongozi wa mrengo huo pekee walihudhuria hafla hiyo Ikulu,” Bw Wambugu aliambia Taifa Jumapili.

Alidai kuwa Dkt Ruto, kiongozi wa ‘Tangatanga’, alishinikiza mgombea wao aidhinishwe na kiongozi wa chama, akiongeza kuwa iwapo Bw Mariga atashinda basi atahudumu kama kibaraka cha kupigia debe kampeni za Naibu Rais wala sio chama cha Jubilee.

“Ingawa Rais alimuidhinisha Bw Mariga kama mgombea wa chama, tunaamini kabisa kwamba Dkt Ruto ndiye alishinikiza kuwepo kwa kikao na Rais ili kupata idhini ya mgombea wake wa ‘Tangatanga’ wala sio wa Jubilee,” alisisitiza.