Habari MsetoSiasa

Uhuru amcheka Maraga kuhusu masaibu kortini

November 6th, 2019 2 min read

VALENTINE OBARA na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne alishindwa kuficha hisia zake kuhusu Idara ya Mahakama, siku moja tu baada ya Jaji David Maraga kutoa msururu wa malalamishi kuhusu anavyodharauliwa na Serikali Kuu.

Rais alikuwa anahutubu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walipaushuru iliyoandaliwa na Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) katika hoteli ya Safari Park, Nairobi alipotambua hotuba aliyokuwa akisoma ilikuwa na sehemu iliyotaja Idara ya Mahakama.

Lakini kabla asome sehemu hiyo, aliinua mikono kama asiyetaka kuhusishwa na kile kilichoandikwa, kisha akashindwa kuzuia kicheko alipotaja Mahakama.

“Kesi nyingi zinazohusu ushuru zimekaa zaidi ya miaka miwili mahakamani na kusababisha changamoto kwa ukusanyaji ushuru. Natoa wito kwa mahakama (akicheka)…wakipenda…wajitahidi kuharakisha uamuzi wa kesi za ulipaji ushuru bila uoga wala mapendeleo,” akasema.

Mnamo Jumatatu, Jaji Maraga alijitokeza katika kikao cha wanahabari kilichodumu zaidi ya dakika 40, akidai kuna njama ya mawaziri na makatibu wa wizara ambao hakuwataja, kumng’oa mamlakani kabla mwishoni mwa mwaka huu.

Mbali na malalamishi yake kuhusu hatua ya Wizara ya Fedha kupunguzia Mahakama bajeti, alilalamika jinsi anadharauliwa serikalini licha ya kuwa yeye ndiye mkuu wa mojawapo ya vitengo vitatu vya serikali vinavyojumuisha Afisi ya Rais, Bunge na Mahakama.

Hisia tofauti zilitolewa na viongozi mbalimbali kuhusu malalamishi hayo, ambapo wengi walitaka Serikali Kuu ikome kukandamiza Mahakama ikiwa na lengo la kuipokonya uhuru wake.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Bw Francis Atwoli alimtaka Rais Kenyatta aingilie kati kukomesha masaibu yanayokumba kitengo hicho cha utekelezaji wa haki.

“Serikali haifai kuingiza siasa katika utoaji haki kwani Wakenya ndio wataumia,” akasema.

Katika Bunge la Taifa, Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) ilikashifu hatua ya wizara ya fedha kupunguza mgao wa fedha kwa Idara ya Mahakama katika mwaka huu wa kifedha ikisema hatua hiyo ilipasa kuidhinishwa na bunge la kitaifa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo William Cheptumo alisema hatua hiyo ni sawa na kuingilia utendakazi wa mahakama kwa kuhujumu utekelezaji wa miradi na mipango yake inayolenga kufanikinisha utoaji haki kwa Wakenya.

Akiongea na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi, Bw Cheptumo pia alisema wizara hiyo ilipasa kutafuta ushauri wa kamati yake kwanza kabla ya kuchukua hatua hiyo.

“Tunafahamu kwamba Wizara ya Fedha ilipunguza bajeti za wizara na idara zote za serikali kuu na kuelekeza fedha hizo katika matumizi mengine kutokana na hali ngumu ya kifedha inayoikumba serikali.

“Lakini hatua hiyo ni kinyume cha sheria kwa sababu hakuidhinishwa na bunge la kitaifa,” akasema Bw Cheptumo ambaye ni mbunge wa Baringo Kaskazini.

Alisema kupunguzwa kwa bajeti hiyo kutaathiri mipango ya idara hiyo ya kujenga mahakama 35 mpya katika maeneo mbalimbali.