Habari

Rais amfokea Kinoti vikali

November 25th, 2020 4 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta amemshambulia vikali kwa maneno Mkurugenzi wa Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI), Bw George Kinoti, kwa hatua yake ya kutaka kufungua uchunguzi upya kuhusu kesi za ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Akionekana mwenye ghadhabu, Rais Kenyatta amesema Jumatano kwamba inasikitisha kuwa kuna watu wanajaribu kuchokora vidonda ambavyo vimepona wakati huu ambapo taifa linaendelea na mchakato wa uponyaji na maridhiano.

“Nilisoma juzi magazetini kwamba kuna wale ambao wanajaribu kuchimbua makaburi kwa kutukumbusha kuhusu yale machafuko ya zamani. Fikiria kabla ya kuongea, fikiria kabla ya kutenda. Siwezi kukubaliana na mambo kama hayo; hatutaki vita,” akasema.

Rais Kenyatta alisema kuwa nia yake ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili taifa hili kwa njia ya kisheria kupitia mageuzi ya Katiba.

“Tunataka kuwaunganisha Wakenya huku tukipalilia amani na umoja,” akasema baada ya kusoma hotuba yake rasmi wakati wa uzinduzi wa shughuli ya ukusanyaji wa sahihi kuidhinisha mageuzi ya katiba kupitia mswada wa BBI.

Rais Kenyatta alisisitiza kuwa hakuwa na habari kuhusu tangazo la Bw Kinoti huku akitoa wito kwa viongozi kukoma kuchochea vita nchini wakati kama huu.

“Hatutaki vita katika taifa letu. Wengine wetu tunajua madhara ya vita na faida ya amani. Hii ndiyo maana tunataka kushughulikia matatizo ambayo huleta shida nchini, kwa njia za kikatiba na kisheria ili Kenya isonge mbele,” akaeleza.

Mnamo Jumatatu, Bw Kinoti alitangaza kuwa afisi yake itafufua kesi za ghasia za miaka ya 2007/2008 na kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika wameadhibitiwa kwa mujibu wa sheria.

Akiongea katika makao makuu ya DCI wakati wahasiriwa 150 wa ghasia hizo walipofika kuandikisha taarifa kuhusu vitisho kuhusu kutokea kwa ghasia zingine, Bw Kinoti alisema polisi watahakikisha kuwa wahusika wameadhibiwa.

Kauli hiyo ilimkera Naibu Rais William Ruto, wandani wake, wazee na viongozi wa kisisa kutoka Rift Valley walimsuta Kinoti kwa kile walichodai ni hatua yake ya kuchochea uhasama wa kikabila katika eneo hilo.

Dkt Ruto na wabunge wandani wake walisema Bw Kinoti anatumiwa na watu fulani kufanikisha mipango ya kuzima ndoto ya Naibu huyo wa Rais kuwania urais 2022, “kwa kumsawiri kama mchochezi wa vita.”

Lakini Jumanne Bw Kinoti alibadili kauli na kukana madai kuwa afisi yake imeanzisha mchakato wa kufufua upya kesi za ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Kwenye taarifa aliyotoa kwa vyombo vya habari, Bw Kinoti alisema hotuba yake Jumatatu, alipokutana na baadhi ya waathiriwa wa ghasia hizo, haikumaanisha kuwa DCI itafungua upya kesi zilizokamilishwa na faili zao kufungwa.

Alisema kile ambacho afisi yake itashughulikia ni malalamishi yaliyoibuliwa na waathiriwa wa fujo hizo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanaishi kwa amani.

Kinoti ajaribu kuzima moto aliowasha

Kinoti alikumbwa na hali ngumu Jumanne akijaribu kuzima taharuki iliyosababishwa na hatua aliyokuwa amechukua mnamo Jumatatu kuhusu kesi za ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa 2007.

Mnamo Jumatatu, Bw Kinoti alikuwa ameitisha kikao cha wanahabari ambapo alitangaza kuwa polisi wanakusanya ushahidi kwa nia ya kuanzisha kesi kuhusu mauaji na visa vingine vya kutisha vilivyotokea wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Hatua hiyo ilikuwa imeibua malalamishi tele, ambapo wanasiasa kutoka mirengo tofauti walidadisi nia ya hatua hiyo kuchukuliwa wakati huu.

Viongozi wanaoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, walidai ni njama za kumhangaisha kisiasa.

Jumanne, Bw Kinoti alikana kuwa afisi yake inataka kufufua upya kesi za ghasia hizo akidai kuwa alipokutana na baadhi ya wahasiriwa wa ghasia hizo, haikumaanisha kuwa DCI itafungua upya kesi zilizokamilishwa na faili zao kufungwa.

Alisema kile ambacho afisi yake itashughulikia ni malalamishi yaliyoibuliwa na wahasiriwa wa fujo hizo kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanaishi kwa amani.

“DCI imepokea malalamishi kutoka kwa umma; watu ambao wanaamini kuwa mali na maisha yao yamo hatarini kutokana na vitisho vinavyoelekezwa dhidi yao. Haya ndiyo mambo ambayo tutachunguza wala si kesi ambazo zilikamilishwa,” Bw Kinoti akasema.

“Ningependa kuwahakikishia Wakenya kwamba tutaendelea kutekeleza wajibu wetu wa kuzuia na kudhibiti uwezekano wowote wa kutokea ghasia popote nchini Kenya. Azma yetu kuu ni kulinda maisha na mali ya Wakenya ambao wameingiwa na hofu kufuatia vitisho vilivyoelekezwa kwao,” akaongeza.

Mnamo Jumatatu, Bw Kinoti aliwapokea zaidi wahasiriwa 120 wa ghasia hizo ambao walifika katika makao makuu ya DCI kuandikisha taarifa kuhusu vitisho ambavyo walidai wamekuwa wakipokea hasa katika maeneo kadhaa ya Rift Valley.

Baada ya kukutana nao, alisema kuwa kesi 72 za mauaji, 144 za kupokonywa ardhi na kesi 118 za vitisho kuhusiana na ghasia ziliandikishwa.

Katika hotuba yake, alisisitiza kuwa kesi za uhalifu huwa hazifungwi hata baada ya muda gani kupita.

Licha ya maelezo aliyotoa Jumanne ambayo yalionekana kujaribu kuzima taharuki iliyosababishwa na matamshi yake ya awali, Naibu Rais alijitosa kwenye mjadala huo.

Dkt Ruto alitaja hatua ya kufufuliwa kwa kesi za ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 kama njama ya kufufua ukabila nchini kuelelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwenye ujumbe kupitia twitter Dkt Ruto alisema hatua hiyo iliyotangazwa na Mkurugenzi wa DCI, Bw Kinoti mnamo Jumatatu, ni njama ya kuhujumu kauli mbiu ya vuguvugu lake la mahasla kwamba “chanzo cha umaskini na ukosefu wa ajira ni uongozi mbaya wala si makabila yetu”.

Wakati huo huo, wabunge wanaounga mkono azma yake ya kuingia Ikulu mwaka wa 2022 waliendelea kumsuta Bw Kinoti.

Wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Bw Kipchumba Murkomen, wabunge hao walidai Bw Kinoti anatumiwa na watu ambao hawakutajwa, kuvuruga amani katika eneo la Rift Valley na “kuzima ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu”.

“DCI anataka kuchochea fujo katika eneo la Rift Valley ili kumsawiri Ruto kama mchochezi wa vita ili azuiwe kuwania urais 2022,” akawaambia wanahabari kikaoni Jumanne katika majengo ya bunge akiandamana na wenzake wapatao 30.

“Tunakataa njama hizo na kutoa wito kwa Wakenya wanaoishi Rift Valley na maeneo mengine nchini kupuuzilia mbali hatua ya Kinoti, na waishi kwa amani,” wabunge hao wakasema kwenye taarifa ya pamoja iliyosomwa na Seneta wa Nakuru, Bi Susan Kihika.

Viongozi hao walimtaka Rais Uhuru Kenyatta amdhibiti Bw Kinoti asije akavuruga azma ya Rais ya kupalilia umoja nchini kabla ya kuondoka mamlakani 2022.