Siasa

Kioni afichua Uhuru sasa ampenda Gachagua

June 4th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KATIBU Mkuu wa chama cha Jubilee Jeremiah Kioni ametangaza kwamba Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ameanza kupendezwa na mbinu mpya za kisiasa za Naibu Rais Rigathi Gachagua ndani ya serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto.

Bw Kioni akihutubia washirikishi wa Jubilee mnamo Jumanne katika Kaunti ya Murang’a, alitangaza kwamba mkutano mkubwa wa kusisitiza wito na maazimio yaliyoafikiwa kwenye kongamano la Limuru III lililoandaliwa mnamo Mei 2, 2024, katika Kaunti ya Kiambu, utaandaliwa katika Kaunti ya Murang’a mnamo Juni 11, 2024.

“Hata mfalme wetu wa siasa, Bw Kenyatta, ameanza kufurahishwa na siasa za Bw Gachagua ambazo zimeanza kuwiana na jinsi alivyokuwa ametuonya kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022. Bw Gachagua sasa ameanza kurejea kwa mkondo wa siasa za Mlima Kenya za kukosoa hali ambapo masilahi yetu yanazidi kudunishwa kila kuchao na utawala wa Kenya Kwanza,” akasema Bw Kioni.

Tangazo hilo la Bw Kioni linaashiria uwezekano wa Bw Gachagua na Bw Kenyatta kuridhiana na kuungana ili kwa pamoja wapalilie umoja wa Mlima Kenya kama ambavyo wamekuwa wakishinikizwa na wadau wa siasa za eneo hilo, wakiwemo wazee wa Agikuyu, Aembu na Ameru.

Bw Gachagua ametumia muda wake mwingi wa Mei 2024 akiomba msamaha hadharani kwa familia ya Hayati Mzee Jomo Kenyatta kutokana na siasa za kuidunisha na kuikosea heshima na hadhi katika kampeni za kabla ya uchaguzi wa mwaka 2022.

Rais Kenyatta wakati huo alikuwa akimuunga mkono kinara wa Azimio La Umoja-One Kenya Bw Raila Odinga huku naye Bw Gachagua akimpigia debe Dkt Ruto aliyekuwa Naibu Rais wakati huo.

Bw Kioni alisema kwamba mkutano wa Murang’a utakuwa wa kuzidisha nduru kwamba “serikali ya Kenya Kwanza inawafuta kazi watu wa kutoka eneo la Mlima Kenya kwa msingi kuwa walikuwa wamepewa nyadhifa hizo na Bw Kenyatta”.

Hayo ni madai yake ambayo Taifa Leo haiwezi kuthibitisha.

“Ni dhahiri serikali ya Kenya Kwanza imeshindwa kutekeleza ahadi yake ya kuinulia wakulima pato la kahawa, parachichi, majanichai na maziwa,” akadai.

Aliongeza kuwa sasa Bw Gachagua ametambua na kuonekana kutubu.

“Alikosea katika mbio zake za kupeleka Mlima Kenya katika ndoa ya kisiasa na Dkt Ruto akiwa hana chama, mkataba rasmi na akikaidi ushauri kutokana na hekima ya Bw Kenyatta,” akasema.

Bw Kioni hata hivyo alisema “hii haimaanishi kwamba sisi tumegeuka kuwa mashabiki wa Bw Gachagua akiwa ndani ya serikali ya Kenya Kwanza yenye uchu wa kuwatoza raia ushuruuliopitiliza”.

“Kile ambacho tunasema ni kwamba sasa tunafaa tuungane hata na huyo Bw Gachagua ili kwa pamoja tuzidi kudai haki yetu ya Mlima Kenya kuhusu ugavi wa rasilimali, uwakilishi sawa katika maeneobunge na pia kuhakikisha chama cha Jubilee hakitekwi nyara na Rais Ruto,” akasema.

Bw Kioni alisema ana imani serikali ya Kenya Kwanza isipojirekebisha kwa kujali masilahi ya raia, basi itakuwa rahisi kuondoka mamlakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.