Uhuru amsaga Ruto Sagana

Uhuru amsaga Ruto Sagana

Na MWANGI MUIRURI

RAIS Uhuru Kenyatta, Jumamosi alimshambulia vikali naibu wake, Dkt William Ruto kwa kupinga mswada wa marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Akihutubia wajumbe takriban 7,000 kutoka eneo la Mlima Kenya katika Ikulu ndogo ya Sagana iliyoko Kaunti ya Nyeri, Rais alikashifu wanaopinga BBI kwa kupotosha wananchi.

Dkt Ruto amekuwa kwenye mstari wa mbele pamoja na wandani wake kupinga BBI inayoongozwa na Rais kwa ushirikiano na kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Rais Jumamosi aliwarai wajumbe hao wa ngome yake ya kisiasa ya Mlima Kenya wapigie debe BBI, na kukanusha kuwa aliwahi kumuahidi Dkt Ruto kurithi cheo chake.

Licha ya kwamba Rais aliwahi kutoa ahadi hiyo mara si moja kwa Dkt Ruto na wafuasi wake, alisema deni alilo nalo ni la maendeleo kwa wananchi pekee.

“Huwa nawasikia wakisema niliwaahidi urithi wa urais… Hapana! Mimi najua tu ahadi yangu ni mkataba na wananchi wote wa Kenya na natekeleza awamu yangu ya utawala nikijitahidi kuwatimizia,” akasema.

Alionekana kughadhabishwa na jinsi naibu wake anavyoendelea kujipigia debe kuhusiana na uchaguzi wa urais wa 2022, badala ya kumsaidia kufanikisha manifesto yao.

“Muulizeni huyo (akiashiria Dkt Ruto) ni kwa nini hataki nifanyie Wakenya kazi. Yeye ameshinda akirudi nyuma kunipokonya kijiti badala asubiri wakati wake ufike. Mtu yeyote ambaye anajali eneo letu na jamii kwa uaminifu lazima atumie mlango wa mbele kuingia. Tujihadhari na wale wanaotaka kutumia mlango wa nyuma au hata dirisha kuingia chumba cha malazi,” akasema.

Mnamo Ijumaa akikutana na madiwani, Rais aliwaambia kwamba jana (Jumamosi) ndipo angefungua roho kuhusu mambo yanayomkera. Na aliposimama kuhutubu, alitimiza ahadi yake.

Alilalamikia jinsi wanasiasa wa kikundi cha Tangatanga kinachoegemea upande wa Dkt Ruto walivyoibua vuguvugu la ‘Hasla’ (walalahoi) huku wakitaka familia za mabwanyenye (dynasty) zisichaguliwe uongozini.

“Utawasikia wakiniita dynasty kwa vile tu nilizaliwa na Kenyatta. Nani huchagua mahali anakotaka kuzaliwa? Waambieni wakome kunitusi, watajua mahali kura hutoka mwaka ujao,” akasema.

Alishangaa kwa nini Dkt Ruto na wenzake wanadai kutetea maskini ilhali walikataa kupitisha mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa kaunti ambao, kulingana naye, ungenufaisha maskini pakubwa.

Alitaja siasa hizo za mrengo wa ‘Tangatanga’ kuwa za unafiki, uongo na tamaa ya uongozi bila kujali athari kwa umma.

“Mnakumbuka jinsi walivyodai kuachwa nje ya handsheki? Si mnakumbuka tukiwa Bomas nilifichua walihusika na hata walikuwa na wawakilishi katika jopo la BBI? Lazima ukweli usemwe. Mbona tusipitishe BBI, kisha tusubiri chochote kile kingine ambacho wanatuahidi baadaye wakiingia mamlakani?” akasema Rais.

Rais alisisitiza kuwa BBI ina nia njema kwa wenyeji wa Mlima Kenya na taifa zima kwa jumla, hasa jamii ambazo zimekuwa zikilalamika kupunjwa na utawala wa Jubilee katika mgao wa fedha za maendeleo.

Aliwahakikishia wenyeji wa Mlima Kenya kuwa angetaka kuwaacha katika nafasi njema kimaendeleo kuliko alivyowapata 2013 alipochukua hatamu za uongozi.

  • Tags

You can share this post!

Leopards, Sharks zapaa ligini huku Sofapaka na wanajeshi wa...

Babayao akunja mkia kufuata Uhuru