UHURU AMTULIZA RAILA

UHURU AMTULIZA RAILA

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi alikuwa mwenye bidii ya mchwa kumtuliza Kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika juhudi za kumshawishi asitoroke handisheki na BBI.

Duru zilieleza kuwa Rais Kenyatta mnamo Jumatano alimtembelea Bw Odinga nyumbani kwake Karen jijini Nairob, ambapo walifanya mkutano kuhusu masuala ya handisheki na BBI.

Kwenye mkutano huo, wawili hao wanaripotiwa kukubaliana kuwathibiti washirika wao walio na misimamo mikali, ambayo inatishia kusambaratisha BBI na handisheki.

Ni kwenye mkutano huo ambapo Rais Kenyatta na Bw Odinga walikubaliana kufanya ziara ya miradi kadhaa jijini Nairobi na Kajiado jana kama mbinu ya kuonyesha kuwa wako pamoja.Duru zilieleza Taifa Leo kuwa wawili hao walikubaliana kuongoza washirika wao kusukuma BBI mbele.

Wadokezi walisema hatua ya Rais Kenyatta kumtembelea Bw Odinga ilitokana na kushtushwa kwake na washirika wa Bw Odinga ambao matamshi yao yameonyesha kuwepo kwa utata kati ya wawili hao.

Jana mchana, rais aliandamana na Bw Odinga kuzuru miradi jijini Nairobi na Kajiado, kisha wakaenda Ikulu pamoja.Awali mnamo Jumanne, rais alimpigia simu kinara wa ODM kumshawishi alegeze msimamo kuhusu masuala ya BBI na handisheki.

Matukio hayo yalionekana kulenga kubembeleza Bw Odinga baada ya kiongozi huyo wa zamani wa upinzani kuonyesha kukasirishwa na jinsi Rais Kenyatta anavyocheza siasa za urithi, pamoja na kutishia kupiga teke mchakato wa kubadilisha Katiba kupitia BBI.

HASIRA

Hasira za Bw Odinga zimetokana na Rais Kenyatta kuonyesha kuunga mkono muungano mpya wa One Kenya Alliance. Muungano huo unajumuisha Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Gideon Moi na Moses Wetangula.

Maafisa wakuu wa ODM nao wamekuwa wakilalamika kuwa maafisa wakuu serikalini wameteka BBI, wakisema hawako makini tena kuisukuma mbele.Hatua ya Rais Kenyatta kupendelea One Kenya Alliance imewauma viongozi wa ODM ambao wanahisi kusalitiwa kwa Bw Odinga, hata baada yake kuwa mwaminifu kwa rais tangu handisheki mnamo 2018.

Katika hatua moja kulizuka kauli za uwezekano wa Bw Odinga kuungana na Naibu Rais William Ruto kukabili One Kenya Alliance, jambo ambalo linaweza kutatiza mpango wa Rais Kenyatta kuhusu anayetaka kuachia madaraka akienda nyumbani 2022.

MAGEUZI YA KATIBA

Kuzuka kwa mvutano katika bunge kuhusu iwapo wabunge wanafaa kubadilisha mswada wa kura ya mageuzi wa BBI, au iwapo unafaa kutekelezwa bila kupigiwa kura kwenye referenda, pia kulitishia kusambaratisha uhusiano rais na Bw Odinga wamekuwa nao kwa kipindi cha miaka mitatu tangu Machi 9, 2018.

Mnamo Jumatano, Rais Kenyatta alimpigia simu Bw Odinga kumhakikishia kwamba hajabadilisha nia kuhusu handisheki na kura ya maamuzi.

Hii ilijiri siku moja baada ya maafisa wakuu wa ODM kulalamika kuwa ofisi ya BBI ilifungwa na vifaa vyote kuhamishiwa ofisi ya Katibu wa Wizara ya Usalama, Karanja Kibicho.

Simu hiyo ilizaa matunda kwani muda mfupi baadaye, Bw Odinga aliitisha mkutano wa Kamati Simamizi ya ODM na kutangaza kuwa handisheki ingali imara na kwamba wanaunga mkonoreferenda.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo ni Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed na Katibu Mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna, ambao wamekuwa wakilalamika kuwa maafisa wakuu serikalini wanapanga siasa za urithi kwa kumzima kiongozi wa chama chao.

You can share this post!

Wandayi akana muungano kati ya Raila na Ruto

Pasaka chungu kwa wakazi wa kaunti tano