Habari Mseto

Uhuru amtuma Muraguri kumaliza mzozo mpakani

August 8th, 2020 2 min read

Na JOSEPH OPENDA

WAKAZI wa maeneo ya Njoro na Marioshoni Kaunti ya Nakuru huenda wakapata suluhu kwa mzozo wa mara kwa mara kati yao, baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati ili masuala yanayozua utata yatatuliwe kabisa.

Rais Uhuru Kenyatta jana alimtuma Katibu wa Wizara ya Ardhi, Dkt Nicholas Muraguri eneo hilo ambalo limekumbwa na mapigano ya kikabila kati ya Wakipsigis na Ogiek tangu wiki jana.

Ziara ya Bw Muraguri inakuja siku chache tu baada ya ghasia zilizotokea wiki jana kusababisha vifo vya watu watano, kuwajeruhi 80 na wengine 3,000 kulazimika kuhama makwao.

Kamishina wa Nakuru Erastus Mbui alisema maafisa wa ngazi ya juu kutoka wizara ya ardhi, maafisa wa misitu na masoroveya, wamekuwa eneo hilo ili waandae mazungumzo na viongozi wa kisiasa kutafuta suluhu kwa mambo yanayosababisha machafuko.

Maafisa hao wa ardhi na misitu watakutana na viongozi 200 kutoka jamii za Ogiek na Kipsigis pamoja na maafisa wa usalama wa Bonde la Ufa wakiongozwa na Kamishna wa ukanda wa Bonde la Ufa George Natembeya katika eneo la Nessuit, kwenye Kaunti ndogo ya Njoro.

Bw Mbui alisema ajenda kuu ya mkutano huo ni kuweka mpaka kati ya ardhi inayofaa kukaliwa na binadamu na msitu na pia kutafuta ardhi mbadala kwa wanaoishi ndani ya msitu.

“Tumekuwa na misururu ya mikutano katika eneo hili na kuwashirikisha viongozi kutoka jamii zote mbili ili kuzima taharuki kati yao. Maafisa wa wizara wamewasili ili kuhakikisha kwamba utata kuhusu mashamba unatatuliwa kabisa,’ akasema Bw Mbui.

Mbunge wa Njoro Charity Kathambi alisema kwamba ana matumaini Bw Muraguri na maafisa wa misitu watapata suluhu kwa mzozo huo wa miaka nenda miaka rudi.

Bi Kathambi pia alishukuru Rais Uhuru Kenyatta kwa kusikiza kilio cha watu hao ili kuhakikisha kwamba amani ya kudumu inapatikana.

“Nina furaha sana kwamba mheshimiwa Rais amesikiza kilio chetu na akachukua hatua. Baada ya mzozo huu kuisha watu wa Njoro wataishi kwa amani na kukumbatia miradi ya maendeleo,’ akasema Bi Kathambi.

Mbunge huyo hata hivyo aliwaomba wanasiasa wajiepushe na kutatiza maafisa wa ardhi na msitu wanaofanya kazi ya kutafuta muafaka kuhusu mzozo huo wa ardhi.

Wakati wa mkutano wa amani ulioandaliwa mnamo Jumatatu, ilibainika kwamba kukosekana kwa mipaka katika ardhi ya misitu, wizi wa ng’ombe na ukosefu wa stakabadhi za kimilili ardhi ni kati ya masuala yaliyochangia vita vya mara kwa mara kati ya Ogiek na Kipsigis.

Huku Wakipsigis wakiwashutumu Ogiek kwa kutumia fujo kuwafurusha kwenye ardhi yao, Ogiek nao waliwalaumu kwa kuwaibia mifugo yao na kuwatetea washukiwa wanaokamatwa.