MakalaSiasa

Uhuru anavyotumia Matiang'i kuzima Ruto

December 5th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

SASA ni wazi kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i ndiye anayetumiwa na Rais Uhuru Kenyatta kumzima Naibu Rais William Ruto kisiasa.

Kikatiba, Dkt Ruto ni msaidizi rasmi wa Rais Kenyatta na inatarajiwa apewe heshima ya wadhifa huo na maafisa wote walio chini yake.

Lakini sasa ni wazi kuwa Dkt Matiang’i anamdharau Dkt Ruto, thibitisho kuwa ana uungwaji mkono kutoka mamlaka makuu ambayo yamo Ikulu.

Hii ilijitokeza wikendi akizungumza katika Kaunti ya Kirinyaga aliposema anatambua mamlaka ya Rais Kenyatta pekee.

“Sisi tunachapa kazi na hatutaki upuzi! Tunafanyia kazi serikali ya Uhuru Muigai Kenyatta na ndiye anayetupatia maagizo pekee. Hakuna nyumba inayoongozwa na wanaume wawili na Kenya inaongozwa na Rais Kenyatta tunayemfanyia kazi,” Dkt Matiang’i alisema akiwa Kirinyaga.

Mdadisi wa masuala ya kisiasa, Martin Andati, anasema akiwa waziri wa usalama wa ndani anayesimamia utawala wa mikoa, Dkt Matiang’i anamwakilisha Rais Kenyatta na kwa hivyo anatoa nguvu zake Ikulu.

Anasema kwamba Dkt Matiang’i anatumiwa kumdoofisha Dkt Ruto kisiasa: “Maafisa wa utawala na polisi wamekuwa wakisusia hafla za Ruto. Ni wazi kuwa ni Uhuru anayezungumza kupitia kwa Matiang’i,” alisema .

Wadadisi wanasema nguvu za Dkt Matiang’i zinadhihirika kutokana na mamlaka aliyopatiwa ya kusimamia kamati za mawaziri kuhusu utekelezaji wa miradi ya serikali, jukumu ambalo kwa kawaida linafaa kuwa la Naibu Rais.

Ikizingatiwa kuwa mkutano wa Kirinyaga ulijiri siku mbili baada ya kuzinduliwa kwa ripoti ya BBI, wadadisi wanasema kauli ya Bw Matiang’i dhidi ya Dkt Ruto ilikuwa ikithibitisha aibu aliyoonyeshwa Naibu Rais katika Bomas.

Katika mkutano huo wa kuzindua ripoti ya Jopokazi la Maridhiano,(BBI), Dkt Ruto alilazimika kusubiri kuondoka baada ya kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga.

Kwa kawaida, Naibu Rais anapaswa kuondoka baada ya Rais lakini maafisa wa polisi walimzuia hadi Bw Odinga akatangulia kuondoka.

“Kwa kawaida, mawaziri wa usalama wa ndani huwa wenye nguvu sana katika utawala wowote ule. Na kwa vile Dkt Matiang’i ameongezewa mamlaka, ni dhahiri kuwa Dkt Ruto amedunishwa,” asema James Warukira ambaye ni mdadisi wa siasa.

Dkt Ruto na wandani wake wamekuwa wakidai kuwa Bw Matiang’i na katibu wa wizara yake Karanja Kibicho wamekuwa wakimhujumu anapotekeleza majukumu yake.

Mnamo Jumapili, Dkt Ruto alimjibu Dkt Matiang’i akimwambia kwamba kazi anayofanya ni ya kuteuliwa tu: “Maafisa wa serikali wanafaa kuwa na heshima kwa wakubwa wao. Hivyo vyeo vikubwa vikubwa mnavyojipiga vifua navyo ni serikali ya Jubilee iliyowapatia,” Dkt Ruto alionya.

Kabla ya kurushiana cheche hizo, Dkt Ruto aliabishwa katika ukumbi wa Bomas wakati maafisa wa usalama, ambao wako chini ya wizara ya Dkt Matiang’i na Bw Kibicho walipokosa kumpa hadhi anayostahili.

Uhasama kati yao ulijitokeza kwanza Dkt Ruto alipokosa kupokelewa na kamishna wa kaunti na wa usalama akiwa katika Kaunti ya Nyeri mnamo Aprili mwaka huu.

Dkt Ruto na wandani wake walimlaumu Bw Matiang’i na Dkt Kibicho kwa kuagiza maafisa hao kususia hafla zake.

Lakini kadri wanavyomkashifu Dkt Matiang’i ndivyo Rais Kenyatta naye anaendelea kumkabidhi mamlaka zaidi kiasi cha kupachikwa wadhifa wa mkuu wa mawaziri.