Uhuru aomba talaka

Uhuru aomba talaka

Na BENSON MATHEKA

TOFAUTI kati ya Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto zinaendelea kuongezeka kiasi cha rais kumtaka Dkt Ruto ajiuzulu.

Uhusiano wa viongozi hao wawili umekuwa baridi tangu 2018 Rais Kenyatta aliposalimiana na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, lakini ni baada ya kuchapishwa kwa mswada wa kura ya maamuzi ambapo walianika tofauti zao hadharani.

Dkt Ruto amekuwa akipinga marekebisho ya katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao ni matunda ya handisheki akisema umelemaza Ajenda Nne Kuu za maendeleo za serikali ya Jubilee.

“Tumeambiwa BBI ndio muhimu kuliko Ajenda Nne Kuu za serikali ya Jubilee kwa sababu inalenga kubuni nyadhifa za uongozi za watu wachache,” Dkt Ruto amenukuliwa akisema mara kadhaa.

Ijumaa, Rais Kenyatta alimwambia Dkt Ruto na wandani wake kwamba wajiuzulu badala ya kukosoa serikali wakiwa ndani.

Akizungumza akiwa Uthiru, Nairobi alipofungua hospitali mpya iliyojengwa na Idara ya jiji la Nairobi (NMS) na mradi wa maji, Rais Kenyatta alimlaumu Dkt Ruto na wandani wake kwa kuendelea kukosoa serikali ilhali wanataka kuendelea kuwa ndani.

“Tunafaa kushirikiana au kutengana. Iwapo wanahisi kwamba serikali inawafaa, basi wanastahili kushirikiana nasi lakini ikiwa wanataka kujitenga nayo, basi wajiuzulu,” Rais alisema.

Dkt Ruto amekuwa akitumia miradi ya serikali kupigia debe azima yake ya urais huku akikosoa handisheki na mapendekezo la kurekebisha katiba.

Licha ya rais kuagiza wanasiasa kusitisha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022, Dkt Ruto amemkaidi na kuendelea kujipigia debe akidai BBI inalenga kumzuia kugombea urais.

Kauli ya rais ya kumtaka ajiuzulu, inatarajiwa kuongeza presha kwa Dkt Ruto ambaye amezuiwa kukanyaga ofisi za chama tawala kufuatia tabia yake ya ukaidi.

Kulingana na katiba ya 2010, Rais hana mamlaka ya kumfuta kazi naibu wake ilivyokuwa katika katiba ya zamani ambapo rais alikuwa na mamlaka ya kumtimua makamu wake.

Kipengele cha 150 cha katiba kinasema kwamba naibu rais anaweza kuondolewa ofisini akipata matatizo ya akili au kupitia mswada bungeni kwa misingi ya utovu wa nidhamu, kukiuka katiba au sheria yoyote ile na kutenda uhalifu chini ya sheria za Kenya na za kimataifa.

Ingawa baadhi ya wabunge wamekuwa wakitisha kuwasilisha mswada wa kumuondoa aondolewe ofisini mchakato wa kufanya hivyo ni mrefu ikiwemo kuungwa na wabunge wasiopungua 233.

Ni ulinzi wa katiba na mahitaji ya kisheria kunakomzuia Rais Kenyatta kumtimua Dkt Ruto na kulazimika kumtaka ajiuzulu.

Ijumaa, Rais Kenyatta alimwambia Dkt Ruto kwamba hafai kujisifu kwa miradi ya serikali anayokosoa.

“Huwezi kutusi watu kwa upande mmoja ukisema serikali ni mbaya na kisha ujisifu kwa mafanikio yake. Ondoka serikalini. Heshima sio utumwa,” alisema ishara kwamba ukaidi wa Dkt Ruto na washirika wake umemfika kooni.

Rais alikosoa kampeni ya Dkt Ruto kupitia vuguvugu lake la hasla na kuitaja kama siasa za pesa nane. “Lengo letu ni kuunganisha Wakenya. Hatutaki siasa duni za mgawanyiko kwa kudai wewe ni tabaka hili au lile,” alisema.

Rais Kenyatta ambaye hajaonekana hadharani pamoja na Dkt Ruto ilivyokuwa awali kabla ya handisheki, alisema yeye anaheshimu watu.

“Mimi ninaheshimu watu. Tukiheshimiana katika serikali, tutapata maendeleo na amani kwa wote,” rais alisema.

Dkt Ruto amelaumiwa kwa kumkaidi na kumdharau rais kwa kutounga BBI na kuendeleza kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022.

You can share this post!

TAHARIRI: Yafaa tuwaruhusu mashabiki viwanjani

CHOCHEO: Utachombeza au kuyatema Valentino hii?