Habari Mseto

Uhuru aomboleza Wachira

October 21st, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ametuma salamu za pole kwa familia, jamaa na marafiki wa aliyekuwa Kamishna wa Polisi Duncan Wachira ambaye alifariki nyumbani kwake Nairobi, Jumatano.

Kiongozi wa taifa amemtaja marehemu kama kama mtumishi wa umma na mzalendo ambayo alijitolea kwa kazi yake kwa faidi ya taifa la Kenya.

“Nimemjua Duncan Wachira kama mtu mwadilifu, mchapakazi na aliyetekeleza majukumu yake kwa kujitolea. Wakati wa hatamu yake kama kinara wa huduma ya polisi, Wachira alianzisha na kutekeleza mageuzi ambayo yaliwasaidia wanaume na wanawake ambao hulinda usalama wetu,” Rais Kenyatta amesema.

Bw Wachira pia anakumbukwa kutokana na jinsi alivyopambana na wahalifu bila ubaguzi wowote, haswa katika jiji la Nairobi.

Rais Kenyatta amesema wakati wa hatamu yake kama Kamishna wa Polisi magenge mbalimbali ya wahalifu yaliweza kusambaratishwa na wanachama wake kuuawa.

Kiongozi wa taifa amesema sifa za Bw Wachira kama afisa aliyejitolea kwa kazi yake itasalia kama mfano mzuri na himizo, haswa kwa vijana ambao wameajiriwa katika vitengo mbalimbali vya usalama nchini Kenya.

Rais Kenyatta ameeleza matumaini yake kwamba Mungu ataipatia familia ya marehemu utulivu na moyo ili iweze kustahimili machungu ya kumpoteza mpendwa wao.