Uhuru aondoa amri ya kutoingia na kutoka kaunti tano zilizofungwa

Uhuru aondoa amri ya kutoingia na kutoka kaunti tano zilizofungwa

Na SAMMY WAWERU

RAIS Uhuru Kenyatta Leba Dei ametangaza kuondoa amri ya ama kuingia au kutoka kaunti tano zilizotajwa kuwa hatari katika maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

Machi 26, 2021, serikali iliweka amri hiyo katika kaunti ya Nairobi, Machakos, Kajiado, Kiambu na Nakuru, kufuatia kile kilisemekana kuwa hatari katika msambao wa virusi vya corona.

Katika hafla ya maadhimisho ya Leba Dei 2021 mnamo Jumamosi, Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuiondoa ila kwa masharti.

“Kuanzia leo (Jumamosi), usiku wa kuamkia Jumapili amri ya ama kuingia au kutoka kaunti tano zilizokuwa hatari katika maambukizi itaondolewa,” akasema Rais Kenyatta, kupitia hotuba yake katika Ikulu, jijini Nairobi.

Aidha, kiongozi huyo wa nchi pia alitathmini saa za kafyu katika kaunti hizo kutoka saa mbili jioni na kutangaza kuwa itakuwa ikianza saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri, sawa na maeneo mengine ya taifa.

“Kwa mujibu wa wataalamu, maambukizi katika kaunti tulizokuwa tumefunga yameshuka kwa asilimia 72, na sehemu zingine za nchi kwa asilimia 89 kati ya Machi 2021 na Aprili,” Rais akaelezea.

Kufungwa kwa kaunti tano zilizoathirika zaidi kulichangia wengi kuhangaika, ikizingatiwa kuwa ni maeneo yanayosaidia kupiga jeki uchumi wa nchi.

You can share this post!

Miaka 10 tangu auawe na Amerika, Osama bado ana ufuasi...

Tottenham wasema hawana haraka ya kujaza pengo la kocha...