Siasa

Uhuru aongoza vigogo wa kisiasa kumpongeza Biden

November 9th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

VIONGOZI mbalimbali nchini jana waliungana na wenzao duniani kumpongeza Rais Mteule wa Amerika, Joe Biden na mgombea-mwenza Kamala Harris, kwa ushindi wao kwenye uchaguzi uliofanyika Jumanne wiki jana.

Kwenye ujumbe wake, Rais Uhuru Kenyatta aliutaja ushindi wa Biden kama dhihirisho la imani ya raia wa Amerika katika uwezo wa uongozi wake

.“Waamerika wamezungumza wazi kupitia kura zao kwa kumchagua kiongozi mwenye tajriba, na anayesifika kote kuwa Rais wao,” akasema kwenye taarifa.“Kwa niaba ya Wakenya wote na Serikali yangu, ninawatakia kila la heri mnapojitayarisha kuchukua usukani kuiongoza Amerika,” akasema Rais, ambaye yuko ziarani Italia.

Rais Kenyatta alimtaja Biden kuwa rafiki wa Kenya, ambaye alisaidia pakubwa kukuza uhusiano wa mataifa hayo mawili kwenye ziara aliyofanya nchini alipohudumu kama Makamu wa Rais wa mtangulizi wake, Barack Obama.

Wengine waliotuma jumbe zao za heri ni Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Seneta Gideon Moi (Baringo) ambaye pia ndiye kiongozi wa Kanu kati ya viongozi wengine.Dkt Ruto aliwapongeza wawili hao akisema wameandikisha historia.

“Heko Joe Biden kwa safari ya imani ambayo imegeuka kuwa ushindi kwa Amerika na dunia nzima. Tunatarajia kuungana nawe kuhutubia hadhira mbalimbali duniani kushughulikia changamoto zinazotukabili. Nakutakia kila heri,” akaeleza Bw Odinga.

Seneta Moi alitaja ushindi wa Biden kama ishara ya kurejea kwa imani katika ulingo wa siasa duniani.Akasema Bw Musyoka: “Heko Biden na Harris. Tunatarajia kukualika Kenya tena hivi karibuni.”

Wengine waliotuma jumbe zao ni kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, magavana Lee Kinyanjui (Nakuru) na Ann Waiguru.