Uhuru aongoza Wakenya kuomboleza Kalembe Ndile

Uhuru aongoza Wakenya kuomboleza Kalembe Ndile

Na MARY WANGARI

RAIS Uhuru Kenyatta aliwaongoza Wakenya kutuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa Kibwezi, Kalembe Ndile katika Nairobi Hospital, Jumapili asubuhi.

Mwanasiasa huyo mcheshi, aliaga dunia Jumapili alfajiri, alipokuwa akifanyiwa upasuaji baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa saratani ya kongosho, kwa mujibu wa mwanawe Anthony Kioko.

Kupitia ujumbe wake wa kuifariji familia, Kiongozi wa Taifa alimwomboleza kigogo huyo wa siasa za Ukambani kama mwanasiasa machachari, mhalisia na ambaye kuinuka kwake maishani kulitokana na bidii yake.

“Inahuzunisha kuwa kifo kimetupokonya mheshimiwa Kalembe Ndile katika umri wake wa makamo. Alikuwa mwanasiasa mchangamfu aliyempenda na kumfanyia kazi kila mtu na ambaye daima alijali maslahi ya taifa,” alisema Rais.

Viongozi wengine wakiwemo Naibu Rais William Ruto, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka vilevile walimwomboleza Bw Ndile aliyefahamika kwa jina lake la utani kama “mtoto wa skwota.”

Akihutubia vyombo vya habari, Bw Musyoka alisema alizungumza na marehemu Jumamosi saa tisa usiku alipokosa kupata nafasi katika Hospitali ya Aga Khan kabla ya kwenda Nairobi Hospital.

Alifafanua kuwa Bw Kalembe hakufariki dunia kutokana na Covid-19 ila kutokana na matatizo kuhusu nyongo ambapo familia inasubiri matokeo kamili kuhusu kilichomuua ghafla.

“Hatujapata habari kamili haswa chanzo cha kifo chake lakini kitu kimoja ninachojua haikuwa Covid-19 kwa hakika lakini kilihusu nyongo. Tutasubiri kupata matokeo halisi kuhusu ni kwa nini alituacha ghafla namna hiyo,” alisema.

You can share this post!

Kafyu kuendelea kwa siku 60 zaidi

Ruto sasa aingia vijijini akilenga kuvumisha UDA