Uhuru aonja kiboko cha Ruto

Uhuru aonja kiboko cha Ruto

AFISA wa polisi wa ngazi za juu aliyekuwa akiongoza walinzi wa Rais (Mstaafu) Uhuru Kenyatta ameondolewa huku aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i akipokonywa baadhi ya walinzi.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba, afisa huyo wa cheo cha Msaidizi wa Inspekta Jenerali wa polisi aliondolewa kwa sababu maafisa wanaomlinda rais mstaafu kisheria wanapaswa kuongozwa na afisa wa cheo cha Inspekta Mkuu.

Hata hivyo, walinzi wa Bw Kenyatta kwa wakati huu wanasimamiwa na supritenda wa polisi, ambaye cheo chake ni cha pili kwa ukubwa kutoka cha Inspekta Mkuu.

Aidha, ilibainika jana kuwa walinzi wa Bw Matiang’i walipunguzwa kutoka 18 hadi wawili huku wale wa aliyekuwa katibu wa wizara ya usalama wa ndani Karanja Kibicho wakipunguzwa hadi wawili kutoka 16.

Walinzi hao huwa wanawasindikiza au kuhudumu katika boma za watu mashuhuri jijini Nairobi na mashambani au katika mali nyingine ya afisa husika.

Haikubainika mara moja kilichosababisha serikali ya Rais William Ruto kuondoa walinzi wa waliokuwa wakuu wa usalama wanaopatiwa kwa kuwa walikuwa wakishikilia nyadhifa muhimu walipokuwa wakihudumu serikalini.

Mabadiliko yaliyofanywa katika walinzi wa Rais mstaafu Kenyatta yalielezwa kuwa yalifaa kuheshimu utaratibu wa vikosi vya usalama kuhusu mamlaka.

Hata hivyo, matukio hayo yalijiri wakati taharuki imetanda kati ya serikali ya Rais Ruto na mtangulizi wake, kufuatia wito wa kuchunguzwa kwa ulipaji ushuru.

Baada ya presha kutoka kwa washirika wa Rais Ruto, Bw Kenyatta alijitokeza Jumanne na kuambia uongozi wa serikali mpya kwamba inafaa kukoma kupayuka na kuzingatia kuhudumia Wakenya.

“Kuna aina mbili za watu. Kuna watu wanaozungumza sana kuhusu watakachofanya na wanakosa kufanya chochote na ni wengi. Lakini kuna watu wa maneno machache na vitendo vyao vinaonekana,” Bw Kenyatta alisema akiwa katika nyumba ya aliyekuwa waziri wake wa elimu, Prof George Magoha, alipoongoza waliokuwa mawaziri katika serikali yake kumuomboleza mwenzao.

Alisema hayo baada ya kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kulaumu serikali ya Ruto kwa kumnyanyasa rais huyo mstaafu, kitu ambacho marais wa zamani, alisema, hawakufanyia watangulizi wao.

Akizungumza katika hafla hiyo Dkt Matiang’i pia alilaumu serikali mpya kwa kupiga kelele. Hatua ya serikali inafuatia kauli kali za viongozi hao wa zamani wa serikali ya Jubilee.

Jana Alhamisi, Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki alikataa kujibu maswali ya Taifa Leo iwapo walinzi wa Rais (Mstaafu) Kenyatta walikuwa wamepunguzwa.

Lakini Bw Kibicho alisema: “Kwanza, katika maisha yangu ya utumishi wa umma, sijawahi kuwa na walinzi 18. Hata nusu ya idadi hiyo. Pili, nilipokabidhi afisi hiyo mnamo Desemba 5, nilirudisha mali yote ya serikali wakiwemo walinzi na magari. Sasa mimi ni raia mwema asiyehitaji walinzi wa kibinafsi.”

Dkt Matiangi na Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome pia hawakujibu maswali ya Taifa Leo.

Alipoulizwa kuhusu kuondolewa kwa afisa wa cheo cha juu wa ulinzi wa rais mstaafu na pia kuondolewa kwa kwa baadhi ya walinzi wa kikosi cha Recce cha GSU pamoja na Dkt Matiang’i na Kibicho kupokonywa walinzi, msemaji wa polisi Dkt Resila Atieno Onyango aliahidi kujibu baada ya saa mbili, lakini hakufanya hivyo.

Rais mstaafu ana haki ya kuwa na walinzi na wafanyakazi wanaolipwa na serikali.

Washirika wa Rais Ruto pia wameapa kuzuia Bw Kenyatta kupata marupurupu yake ya kustaafu akiendelea kushikilia wadhifa wa mwenyekiti wa Baraza Kuu la muungano wa upinzani wa Azimio la Umoja One Kenya.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yakemewa njaa ikiwadia tena

Papa Francis ahubiri msamaha, maridhiano

T L