Uhuru aonyesha Raila Ikulu

Uhuru aonyesha Raila Ikulu

CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta, jana Jumapili alionyesha wazi kwamba anamuunga kiongozi wa ODM Raila Odinga kuwa mrithi wake kwa kumkweza mbele ya Naibu Rais William Ruto katika maadhimisho ya Jamhuri Dei.

Rais Kenyatta alimmiminia sifa Bw Odinga kiasi cha kuvunja itifaki na kumwalika kuhutubu baada ya kusoma hotuba yake rasmi kwa taifa.

Katika tamko lililoonyesha wazi kwamba amekuwa akimshika mkono kumwelekeza njia ya kuingia Ikulu baada ya uchaguzi mkuu ujao, Rais Kenyatta alidokeza kwamba amekuwa akitembelea mradi wa kijeshi akiandamana na kiongozi huyo wa ODM.

Rais Kenyatta ndiye Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Kenya na shughuli zote za kijeshi, ikiwemo miradi inayotekeleza, huwa haziko wazi kwa raia.

Hivyo basi, kufichua kwamba amekuwa akipata ushauri na kuandamana na Bw Odinga kukagua mradi unaotekelezwa na jeshi, ni ishara kwamba anamwamini na kumtakia makubwa.

“Nachukua fursa hii kuwashukuru wote tulioshirikiana nao katika ujenzi wa bustani ya Uhuru Gardens. Nitakosea ikiwa sitataja mtu mmoja ambaye mara kadhaa tulitembea hapa na nimekuwa nikishauriana naye kwa miezi 14 iliyopita nilipoanza mradi huu, na ambaye alinipa ushauri. Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, nasema asante sana kwa hili,” Rais Kenyatta akasema.

“Sasa najua hawa wazee wangependa useme machache. Karibu,” akaongeza huku akivunja itifaki kwa kumwalika Bw Odinga ahutubie Wakenya.

Kauli hiyo ilionekana kama kumweka Bw Odinga katika hadhi ya juu kuliko viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kitaifa akiwemo Naibu Rais William Ruto.

Dkt Ruto ambaye ndiye mshindani mkuu wa Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais 2022, ameonekana kutengwa serikalini tangu Rais Kenyatta na Bw Odinga walipozika tofauti zao kupitia handisheki 2018.

Katika hotuba yake rasmi Rais Kenyatta alisema alikubali kuzika tofauti za kisiasa na Bw Odinga mnamo Machi 9, 2018 ili kuendeleza umoja ambao waanzilishi wa taifa hili walianzisha 1963.

“Tulifanya handisheki na ndugu yangu Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa sababu tuliona nyufa katika ukuta wa taifa letu. Tulitaka kuziba nyufa hizo ili kupalilia umoja wa kitaifa jinsi tulivyoshauriwa na mababu zetu,” akaeleza.

Hii sio mara ya kwanza kwa Rais Kenyatta kuvunja itifaki na kumpa Bw Odinga nafasi ya kuhutubia katika hafla za kitaifa.

Mnamo Oktoba 20, 2021, Rais alimpa Bw Odinga nafasi kuhutubu katika Sikukuu ya Mashujaa katika uwanja wa Wang’uru, kaunti ya Kirinyaga.

Hadhi ambayo Rais Kenyatta alimpa Bw Odinga jana Jumapili inajiri siku mbili tu baada yake kutangaza rasmi kwamba atawania urais katika uchaguzi mkuu ujao.

“Mimi Raila Amollo Odinga, kwa kujitolea kujenga Kenya ninaheshimu misingi ya kidemokrasia na maendeleo, na kwa kushirikiana na Wakenya wazalendo waliojitolea kufikia lengo hili, najiwasilisha kama mgombeaji wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 kufuatia ombi na idhini ya mkutano huu wa Azimio la Umoja,” akasema huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wafuasi wake waliofurika katika uwanja wa michezo wa Kasarani, Nairobi.

Karibu mawaziri saba wa serikali walihudhuria mkutano huo ishara kwamba walipata idhini kutoka kwa bosi wao, Rais Kenyatta.

Miongoni mwao walikuwa; Joe Mucheru (ICT), Sicily Kariuki (Maji), Peter Munya (Kilimo), Keriako Tobiko (Mazingira), Ukur Yatani (Fedha) na Eugene Wamalwa (Ulinzi).

Siku moja kabla ya mkutano huo, bwanyenye kutoka Mlima Kenya, chini ya mwavuli wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF), waliunga mkono azma ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu 2022.

Kundi hilo lenye ushawishi mkubwa kisiasa na kiuchumi katika eneo la Mlima Kenya lina uhusiano wa karibu zaidi na Rais Kenyatta.

Wanachama wa MKF walipiga jeki kampeni za Rais Kenyatta na Dkt Ruto katika chaguzi za 2013 na 2017.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali iingilie suala la mzigo unaobebeshwa...

Mshukiwa mmoja akamatwa, polisi wapata lita 38 za pombe...

T L