Habari za Kitaifa

Uhuru apiga vijembe Kenya Kwanza akiifananisha na usaliti wa Judas Iscariot

April 8th, 2024 2 min read

NA COLLINS OMULO

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amefufua siasa za usaliti nchini baada ya kushambulia wanasiasa aliowataja kama “wasaliti”

Bw Kenyatta, ambaye katika miezi kadha iliyopita amejiepusha na siasa, alisema hayo alipohudhuria hafla ya kutawazwa kwa Maaskofu wasaidizi wateule Simon Peter Kamomoe na Wallace Ng’ang’a Gachihi katika uwanja wa Kanisa Katoliki la St Mary’s Masongari, Nairobi, Jumamosi, Aprili 6, 2024.

Akirejelea mahubiri ya Mwakilishi wa Papa Nchini, Askofu Mkuu Matheus Maria Van Megen yaliyohusu usaliti kanisani, Bw Kenyatta alishambulia watu ambao hakuwataja akisema hawatapiga hatua kwa kuwa wasaliti.

“Askofu Mkuu ameongea kuhusu wasaliti kanisani lakini nataka kusema kuwa sioni wasaliti wengi kanisani. Usaliti umekithiri upande ule mwingine (huku akionyesha upande walipoketi wanasiasa),” akasema Bw Kenyatta.

“Kwa wasaliti, ninataka kuwaambia kuwa hata Judas (Iscariot) alimsaliti Yesu lakini baadaye aliacha pesa na kujitia kitanzi. Kila kitu kina mwisho,” akaongeza.

Akiendeleza shambulio lake, Rais huyo Mstaafu alisema kwa muda mrefu watu wamechukulia uongozi kumaanisha “uwezo wao wa kuwakalia watu wengine.”

“Jinsi Askofu Mkuu ametukumbusha leo, wajibu wa mchungaji sio kuamuru bali kuongoza na kuleta watu wote pamoja nawe,” akasema Bw Kenyatta.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Jaji Mkuu Martha Karua, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, Mawaziri; Moses Kuria na Susan Nakhumicha, Waziri wa Zamani Monica Juma na wanasiasa wa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio.

Miongoni mwao walikuwa ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, na wabunge Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini) na Tim Wanyonyi (Westlands).

Hii sio mara ya kwanza kwa Bw Kenyatta kuzunguzia usaliti wa kisiasa baada ya kutofautiana na aliyekuwa naibu wake, sasa Rais William Ruto, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mnamo Julai mwaka jana, 2023, Bw Kenyatta alikasirika na kumtaka Rais Ruto akimkabili na amkamate ikiwa amevunja sheria yoyote.

Alisema hayo alipolaani tukio ambapo maafisa wa usalama walivamia makazi ya mwanawe Jomo katika mtaa wa Karen wakidai walikuwa wakisaka bunduki haramu.

Bw Kenyatta alimwonya Ruto dhidi ya kuhangaisha watu wa familia na badala yake akabiliane naye moja kwa moja.

Aidha, Rais huyo mstaafu alitaja kisa ambapo walinzi katika makazi ya mamake, Mama Ngina Kenyatta mtaa wa Muthaiga na Gatundu Kusini waliondolewa bila nyanya huyo kufahamishwa.

Alitaja hatua hiyo kama sehemu ya njama “mbovu” ya serikali kutumia vyombo vya dola kumhangaisha na familia yake.

Wakati huo, Rais Ruto alikuwa amedai mara si moja kwamba Bw Kenyatta ndiye alikuwa akidhamini na kufadhili maandamano ya wafuasi wa Azimio ya dhidi ya serikali yake.

Aidha, Bw Kenyatta alishambuliwa vikali na aliyekuwa msaidizi wake na sasa Naibu Rais Rigathi Gachagua baada ya wawili hao kutofautiana vikali kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Aidha, wanasiasa waliokuwa wandani wake kuelekea uchaguzi huo sasa wamegeuka kuwa mahasidi wake na wanashirikiana na maadui wake kisiasa.

Miongoni mwao ni Mbunge Maalum Sabina Chege na Mwakilishi wa Kenya katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kanini Kega ambao sasa wanashirikiana kisiasa na Rais Ruto na Bw Gachagua.