Habari

Uhuru ashauri viongozi wa Pwani waungane

September 7th, 2019 1 min read

Na PSCU Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa viongozi wa eneo la Pwani kuungana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.

Rais alishauri vingozi hao wawe na mawazo pana na mtazamo wa kudumu wa maendeleo akisema wanastahili kuzingatia miradi ambayo itawanufaisha watu wengi zaidi kupitia kuchuma mali na kubuni nafasi za kazi.

Rais ambaye alizungumza katika Ikulu ya Mombasa alipowapokea viongozi waliochaguliwa kutoka eneo hilo, aliwashauri viongozi hao kila mara kuzingatia maslahi ya wananchi badala yale ya kibinafsi.

“Tutafute suluhisho kwa changamoto zetu, hakuna jambo lisilowezekana iwapo tutaungana,” Rais Kenyatta aliwaambia viongozi hao wakiwemo Magavana sita wa kaunti za Pwani: Mombasa, Kilifi, Lamu, Taita Taveta, Kwale, na Tana River.

Rais alisema wakati umewadia kwa viongozi kufikiria jinsi watakavyokumbukwa na kizazi cha sasa na kile kijacho.

“Sharti tukadirie historia yetu kama taifa na pia kama eneo, na tujiulize iwapo watu wetu kama Wakenya wanaweza kuendelea kudumisha siasa za utengano, siasa za chuki, siasa za kuhujumiana na bado tuamini kwamba tutafaulu kuwa taifa lenye mapato ya kiwango cha kadri itimiapo mwaka 2030. Inawezekana kweli?” Rais akauliza.

Kuhusu maendeleo, Rais alibainisha baadhi ya miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali yake katika eneo hilo akiongeza kwamba Serikali itahakikisha utekelezaji wa miradi yote inayoendelea ikiwemo barabara, maji na miundomsingi mingine inakamilishwa.

Uwekezaji

Alisema miradi kama ile ya ujenzi wa barabara kadhaa, Eneo Maalum la Kiuchumi la Dongo Kundu na Bandari ya Lamu inanuiwa kufungua eneo hilo kwa uekezaji zaidi.

Viongozi wote waliozungumza katika mkutano huo wa mashauriano wakiwemo magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Salim Mvurya (Kwale), Amason Kingi (Kilifi), Dhadho Godhana (Tana River), Fahim Twaha (Lamu) na Granton Samboja (Taita Taveta) walisema wanaunga mkono ajenda ya maendeleo ya Rais kulingana na ajenda kuu ya nguzo nne za maendeleo.