Uhuru ashikilia ufunguzi wa Bunge la Kitaifa

Uhuru ashikilia ufunguzi wa Bunge la Kitaifa

SAMUEL OWINO Na DAVID MWERE

RAIS Uhuru Kenyatta ameshikilia ufunguo wa Bunge huku Rais Mteule William Ruto naye akimezea mate viti vya uspika katika Mabunge ya Kitaifa na Seneti.

Ishara zote zinaonyesha kuwa Rais Kenyatta ambaye kisheria anastahili kuamrisha siku na tarehe ya wabunge wapya kuapishwa, huenda asifanye hivyo kabla ya Mahakama ya Juu kutoa uamuzi kwenye kesi inayotarajiwa kuwasilishwa na Raila Odinga. Kesi hiyo itakuwa ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto.

“Baada ya wabunge wapya kuchaguliwa, Rais kupitia notisi kwenye gazeti atateua siku na mahali ambapo kikao cha kwanza kitaandaliwa. Muda huo haustahili kuchukua siku 30 baada ya uchaguzi kukamilishwa,” inasema Ibara ya 126 (2) ya katiba.

Sheria inaipa Azimio siku saba kuwasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Dkt Ruto ambazo zinakamilika Jumatatu. Iwapo watawasilisha kesi siku hiyo, basi Majaji wa Mahakama ya Juu watachukua siku 14 kusikiza na kuamua kesi hiyo ambayo inaishia Septemba 6.

Hapo jana, Kaimu Karani wa Bunge Serah Kioko alichapisha kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa kutakuwa na kikao mnamo Alhamisi na Ijumaa wiki ijayo katika majengo ya bunge.

Kikao hicho kitakuwa cha kuwapa wabunge mafunzo jinsi watakavyojiapisha baada ya Rais Kenyatta kuweka wazi tarehe ya uapisho.

Majina ya wabunge hao yatasajiliwa, maelezo kuwahusu yanakiliwe, wapokezwe kadi za utambulisho bungeni na pia wafundishwe jinsi ya kupiga kura kwa mfumo wa kielektroniki.

Pia watatembezwa ndani ya bunge na kuarifiwa na makarani kuhusu mchakato wa kisheria wa kuwasilisha hoja mbalimbali.

“Wabunge wateule watasaidiwa wajisajili ili kunufaikia huduma mbalimbali ikiwemo bima ya matibabu na manufaa mengine yanayoandamana na kuwa mbunge,” akasema Bi Kioko.

Wabunge hao wateule wanastahili kubeba kitambulisho au pasipoti, nambari ya Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA), cheti walichopokezwa cha ushindi kutoka kwa IEBC na pia wasifu kazi.

Hata wabunge ambao wamechaguliwa tena wanastahili pia kuleta stakabadhi hizo.

Bi Kioko aliwataka hata wale ambao walikuwa wakihudumu hapo awali wahudhurie vikao hivyo kwa sababu hapo ndipo makarani na wafanyakazi wengine wabunge hupata nafasi ya kujibu maswali yao.

Hata hivyo, maeneobunge manne ya Kacheliba, Kitui Mashambani, Rongai na Pokot Kusini hayatakuwa na wawakilishi kwa sababu IEBC iliahirisha uchaguzi katika maeneo hayo.

Haya yanajiri wakati ambapo Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ameonya kuwa hatua ya Tume ya Kuoanisha Mishahara Nchini (SRC) kufuta marupurupu ya wabunge wakihudhuria vikao, kutapunguza idadi yao wanaofika kuwajibikia miswada mbalimbali.

Wabunge wote 349 walikuwa wakilipwa Sh5,000 , pesa ambazo maseneta wote 67 pia walikuwa wakipokea kulingana na notisi ya gazeti la SRC iliyochapishwa Machi 1, 2013.

Notisi ya gazeti iliyofuta marupurupu ya vikao ilianza kutekelezwa rasmi baada ya uchaguzi mkuu wa wiki jana.

  • Tags

You can share this post!

Kura moja tu yamwingiza bunge la kaunti

Korti ya Juu yakataa barua ya mpigakura

T L