Majaji: Uhuru ashinda raundi ya kwanza

Majaji: Uhuru ashinda raundi ya kwanza

Na RICHARD MUNGUTI

RAIS Uhuru Kenyatta ameshinda raundi ya kwanza kwenye mzozo kuhusu uteuzi wa majaji sita, baada ya Mahakama ya Rufaa kusimamisha kwa muda agizo la kuwaapisha ndani ya siku 14.

Majaji Roselyn Nambuye, Wanjiru Karanja na Imana Laibuta walikanyagia breki agizo kwamba Rais Kenyatta awaapishe majaji sita aliokataa kuwalisha kiapo cha afisi tangu 2019.

Baada ya kukataa kuwaapisha sita hao, Rais Kenyatta aliwasilisha rufaa kupinga agizo la majaji watatu wa Mahakama Kuu, akidai ana habari kwamba sita hao walikuwa wamehusika na visa vya ufisadi.

“Baada ya kutilia maanani ushahidi uliowasilishwa, rufaa ya mwanasheria mkuu iko na uwezekano mkubwa wa kufaulu,” walisema majaji hao.

Majaji wa mahakama kuu George Dulu, William Musyoka na James Wakiaga waliamuru kwamba, iwapo Rais Kenyatta atakawia kuwaapisha majaji hao sita, Jaji Mkuu Martha Koome awaapishe mwenyewe.

Agizo hilo kwamba Rais Kenyatta awaapishe majaji hao sita lilitolewa wiki mbili zilizopita.Majaji hao ni Joel Ngugi, Weldon Korir, Aggrey Muchelule na George Odunga.

Majaji hao wanne walikuwa waapishwe kujiunga na Mahakama ya Rufaa ilhali hakimu mkuu Evans Makori na naibu wa msajili wa Mahakama Kuu Judith Omange waliteuliwa kuwa majaji katika kitengo cha kuamua kesi za mashamba cha mahakama kuu.

Majaji Nambuye, Karanja na Laibuta waliamuru majaji hao waendelee kutekeleza majukumu yao katika mahakamka kuu kabla ya kuamuliwa kwa rufaa iliyowasilishwa na mwanasheria mkuu Paul Kihara Kariuki.

Agizo hilo la kusitisha kuapishwa kwa sita awa yamaanisha watendelea kutekeleza majukumu yao.Majaji hao Nambuye, Karanja na Laibuta watatoa sababu kamili za kusitisha uapishaji hao hadi Novemba 19, 2021.

“Kwa sasa tutatangaza tu agizo la muda lakini tutatoa sababu kamili za kusitisha kuapishwa huko mnamo Novemba 19, 2021,” likasema agizo la majaji Nambuye, Karanja na Laibuta.

Agizo hilo lilifuatia rufaa iliyowasilishwa na Bw Kihara aliosema majaji wa mahakama kuu walijitwika majukumu wasiyo nayo ya kumshurutisha Rais kuwaapisha majaji hao na pia kumpa Jaji Mkuu Koome kutekeleza jukumu lisilo lake la kuwaapisha majaji haosita walioteuliwa 2019 na tume ya huduma za mahakama JSC kujiunga na mahakama ya rufaa na mahakama kuu.

You can share this post!

MKU na Unesco kushirikiana kufanikisha mradi wa afya wa o3...

Ruto ataka wapinzani waje na sera zao

T L