Uhuru asukuma Ruto, Raila kona moja

Uhuru asukuma Ruto, Raila kona moja

WANDERI KAMAU na BENSON MATHEKA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kuonekana kupendelea muungano mpya wa ‘One Kenya Alliance’ imewasukuma naibu wake William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kona moja kisiasa.

Kwa kuhisi kusalitiwa na Rais, wawili hao wameanza kuelekeza makombora kwa muungano huo unaoshirikisha Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka, Gideon Moi na Moses Wetangula, wakiutaja kama unaogawanya Wakenya kikabila badala ya kuwaunganisha kupitia vyama vyenye sura ya kitaifa.

Alhamisi, Dkt William Ruto alisema yuko tayari kufanya kazi na Bw Odinga, akieleza kuwa tofauti zao ni za kisiasa, lakini hilo halimaanishi hawawezi kushirikiana.

“Baadhi ya watu hudhani nina tatizo na Bw Odinga. Huo si ukweli. Tofauti hizo ni za kisiasa. Hata hivyo, kuna mambo ninayokubaliana naye, kama vile kubuniwa kwa vyama vya kisiasa vya kitaifa. Anakabiliwa na changamoto sawa ninazokumbwa nazo kutoka kwa viongozi wa kikabila. Tunaweza kushirikiana na kufanya kazi pamoja,” akasema Dkt Ruto.

Wawili hao wamekuwa maadui sugu kisiasa hasa kuhusu handisheki na BBI, lakini muungano wa ‘One Kenya Alliance’ umejitokeza kuwa kifaa kinachowaleta pamoja.

Matamshi ya Dkt Ruto jana yalitokea katika kipindi ambapo viongozi wanaoegemea mrengo wake chini ya chama cha United Democratic Alliance (UDA), wamekuwa wakijiegemeza upande wa wandani wa Bw Odinga bungeni.

Mnamo Ijumaa, maseneta wanaoegemea UDA waliunga mkono hatua ya ODM ya kumpokonya Seneta wa Kakamega, Cleophas Malala wa ANC wadhifa wa kiongozi wa wachache katika Seneti.

Maseneta wa ODM nao wamekubaliana na washirika wa naibu rais, kwamba bunge lifanyie mabadiliko mswada wa BBI hasa kipengele kuhusu maeneobunge mapya, jambo ambalo limepingwa na Jubilee.

Hivi majuzi, Seneta wa Siaya, Bw James Orengo aliongoza wandani wengine wa Bw Odinga kukashifu watumishi wa umma ambao wanadaiwa kula njama ya kuiba kura za urais 2022. Malalamishi kama haya yamekuwa yakitolewa kwa muda mrefu na Dkt Ruto.

Alhamisi, ODM ilidokeza uwezekano wa kuunda muungano wa kisiasa, ambao ilisema hautarajiwi na wengi.

“Rekodi yetu ya kuunda miungano, kujenga daraja na wanaochukuliwa kuwa maadui wetu na kuwakuza viongozi vijana wenye nguvu inajulikana. Kwa mara nyingine, tunapanga kufanya hivyo,” alisema Katibu Mkuu Edwin Sifuna.

Sawa na Dkt Ruto, Bw Sifuna alipuuzilia mbali “Kenya Moja Alliance” akiutaja kama muungano wa kikabila.

Wadadisi wa siasa wanasema si vigumu kwa Dkt Ruto na Bw Odinga kushirikiana tena kisiasa, kwani waliwahi kuwa pamoja katika ODM mnamo 2007, kupitia kundi la ‘Pentagon.’

“Hawa ni wanasiasa wenye uzoefu mkubwa. Wanafahamiana kwa undani kwani washawahi kuwa pamoja hapo awali. Huenda isiwe vigumu kwao kuungana tena,” akasema mchanganuzi wa siasa Javas Bigambo, kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Lakini washirika wa ‘One Kenya Alliance’ wamejitetea wakisema wao ndio wa kuaminika kutatua changamoto zinazokumba nchi.

Katika kikao cha wanahabari jana, viongozi hao walidai ODM imethibitisha haiwezi kuaminika kwa kukiuka makubaliano ya awali katika muungano wa NASA ambapo vyama tanzu husisitiza kulikuwa na makubaliano Bw Odinga asiwanie urais tena 2022.

“Leo tunaanza safari tukiwa na lengo la kuunganisha nchi kupitia ajenda ya mabadiliko ambayo itabuni nafasi kwa Wakenya wote. Muungano huu ni pumzi safi kutoka kwa siasa za migawanyiko ambazo nchi imekuwa ikishuhudia,” akasema Bw Musyoka.

Muungano huo pia ulitangaza utaunga mkono wawaniaji wa ODM kwenye chaguzi ndogo dhidi ya wale wa ODM.

Matukio haya yanatarajiwa kutatiza juhudi za Rais Kenyatta kuleta pamoja vigogo wote wa kisiasa dhidi ya Dkt Ruto.

You can share this post!

Uhispania wakabwa koo na Ugiriki

Wizara yawataka wanasiasa wajitokeze kwa chanjo ya corona...