Habari

Uhuru atabaki katika uongozi baada ya 2022, adai Murathe

December 30th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa chama cha Jubilee, Bw David Murathe amesisitiza kwamba kuna uwezekano mkubwa Rais Uhuru Kenyatta atasalia katika uongozi mkuu wa taifa hata baada ya 2022.

Kwenye mahojiano ya kipekee na ‘Taifa Leo’, Bw Murathe alisema ikizingatiwa kwamba mfumo wa uongozi unatarajiwa kubadilishwa kupitia kwa jopo la maridhiano (BBI), Rais Kenyatta atasalia mamlakani kwa njia nyingine kama vile kushikilia wadhifa wa Waziri Mkuu.

Bw Murathe ambaye hutazamwa kama anayefahamu mengi kuhusu mipango inayoendelezwa serikalini kisiasa, alisema kufikia sasa ni wazi kwamba BBI itatoa nafasi moja ya uongozi wa taifa kwa kiongozi wa chama au muungano utakaokuwa na wengi bungeni.

Rais Kenyatta ndiye kiongozi wa Chama cha Jubilee ambacho kwa sasa ndicho chenye wabunge wengi wa kitaifa.

“Rais haruhusiwi tu kuwania urais lakini chini ya mfumo mpya unaotarajiwa kupitia kwa ripoti ya BBI, patakuwa na nafasi zaidi za uongozi. Hakuna chochote kitakachomzuia Rais aliye kiongozi wa Jubilee kusimamia serikali kama Waziri Mkuu mwenye mamlaka, mradi tu chama hicho kiendelee kuwa kikubwa zaidi kwa idadi ya viongozi nchini Kenya,” akasema.

Wakatii Rais alipohutubia viongozi wa Jubilee na wengine kutoka Mlima Kenya mnamo Novemba, alisema, ijapokuwa kwa utani, kwamba akipewa wadhifa huo hatakataa.

Suala la uwaziri mkuu ni mojawapo ya yale yanayoendelea kuibua joto la kisiasa nchini.

Hivi majuzi, chama cha ODM ambacho kimekuwa katika mstari wa mbele kupigania wadhifa wa Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa, kilijitokeza na kusema kuwa kitaacha uamuzi huo mikononi mwa wananchi.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa walichukulia hatua hiyo ya kubadili msimamo kumaanisha chama hicho kimetambua kuwa kuwepo kwa wadhifa huo hakutamaanisha utaenda moja kwa moja kwa kiongozi wao, Bw Raila Odinga.

Hii ni kutokana na kuwa, ili ODM ipate wadhifa huo, itahitajika iwe na idadi kubwa ya wabunge kama chama au kupitia kwa muungano wa vyama tanzu, suala ambalo ni kizungumkuti kisiasa.

Vile vile, imesemekana kuna viongozi wa ODM ambao wanaamini bado Bw Odinga ana nafasi ya kuwania urais na hivyo basi, haitakuwa busara kupigania mamlaka zaidi yatolewe kwa uwaziri mkuu kuliko Rais chini ya mfumo mpya unaotarajiwa kupitia kwa BBI.