Habari Mseto

Uhuru ataka IFMIS iwekwe kaunti zote

June 25th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Rais Uhuru Kenyatta ameagiza Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia(ICT) kuzindua mfumo wa kusimamia matumizi ya fedha (IFMIS) katika kaunti zote.

Rais Ijumaa alisema mfumo huo utasaidia katika kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha na uwazi katika matumizi ya fedha za umma.

Rais Kenyatta aliitaka wizara hiyo kutumia njia zote kuhakikisha kuwa kaunti zote zimeunganishwa na mfumo huo.

Serikali inajitahidi kuunganisha maeneo yote na mfumo wa kisasa wa intaneti, hivyo, itakuwa rahisi kwa mfumo wa IFMIS kufanya kazi.

“Hili sio suala linaloweza kungoja, na tunawataka kuunganisha maeneo yote na intaneti, kuweni wabunifu,” alisema alipokutana na waratibu wa baraza la magavana na maafisa wa serikali, Ikulu, Nairobi.

Kulingana na Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia Joe Mucheru, sio tu wizara yake itasambaza mfumo wa intaneti kwa makao makuu ya serikali za kaunti, itasambaza mfumo huo kote nchini.