Habari MsetoSiasa

Uhuru atamuunga mkono Ruto 2022 – Mwaboza

April 14th, 2019 1 min read

Na SAMUEL BAYA

BAADHI ya wanasiasa wa chama cha Jubilee kutoka eneo la Pwani wamesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta hajabadili msimamo wake wa kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2022.

Mbunge wa zamani wa Kisauni, Bw Anania Mwaboza na mwenyekiti wa mipango katika chama hicho Kaunti ya Kilifi, Bw Alwy Sharrif wanasema Rais Kenyatta hajawahi kujitokeza wazi na kusema kwamba hatamuunga mkono Dkt Ruto.

Hata hivyo, wawili hao walidai kuwa kuna njama ya baadhi ya viongozi wa Jubilee kutaka kumzuia Naibu wa Rais kuwa rais mwaka wa 2022.

Wakizungumza katika mahojiano na mwandishi wetu, wanasiasa hao walisema kuwa masaibu ya chama hicho yamechochewa na watu chamamni ambao lengo lao ni kuona kuwa Bw Ruto hapati nafasi ya kuwania urais baada ya Rais Uhuru kuondoka mamlakani.

Bw Mwaboza alisema madai yote ambayo yamekuwa yakitolewa na wanasiasa wa Jubilee wanaompinga Naibu Rais yanalenga kumchafulia sifa ili kumkosesha urais 2022.

“Rais Uhuru Kenyatta mwenyewe aliwahi kusema hadharani kwani baada ya yeye kuondoka uongozini, Bw Ruto angechukua nafasi hiyo. Huo ndio mkataba kati ya viongozi hao wawili na hatuoni haja kamwe ya kubadilisha maneno,” akasema Bw Mwaboza.