Habari Mseto

Uhuru atangaza mabadiliko serikalini

August 23rd, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Masuala ya Ndani Fred Matiang’i na mwenzake wa Maji Simon Chelugui wameongezwa mamlaka katika mageuzi ndani ya serikali ambayo Rais Uhuru Kenyatta ametangaza Ijumaa.

Naye Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri alipunguziwa mamlaka baada ya idara ya Unyunyiziaji kuondolewa kutoka Wizara yake na kupelekwa katika Wizara ya Maji.

Dkt Matiang’i sasa atasimamia Idara ya Uhamiaji na Huduma za Rais pamoja na Kitengo cha Utekelezaji wa Shughuli za Serikali na Idara ya Uwiano wa Kitaifa.

Na baada ya Idara ya Unyunyiziaji kuondolewa kutoka Wizara ya Kilimo, sasa Bw Chelugui atasimamia Wizara inayojulikana kama Wizara ya Maji, Usafi na Unyunyiziaji.

Bw Kiunjuri anasalia na wizara ijulikanayo kama Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

“Serikali yangu imefanya mabadiliko haya ili kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma katika wizara, idara na mashirika ya serikali,” akasema Rais Uhuru Kenyatta katika agizo la kiserikali alilotoa Ijumaa.

Mabadiliko hayo yanaanza kutekelezwa mara moja.