HabariSiasa

Uhuru ategwa na wanyakuzi wa ardhi

February 27th, 2018 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

Kwa ufupi:

  • Wakuu serikalini wanahakikisha wanamiliki vipande vya ardhi katika shamba la ekari 40,000 viungani mwa jiji la Nairobi
  • Njama ya kuingilia shughuli hiyo inashirikisha watu 2,500 walionunua hisa katika kampuni hiyo kwa njia za ulaghai kisha wakajitwalia ardhi
  • Sababu kuu ya matatizo ya uhalalishaji wa umiliki ulioagizwa na Rais Kenyatta ni kuwa walionunua hisa kwa ulaghai wanahudumu katika ngazi za juu serikalini
  • Wenyehisa halali wanafaa kuwa 13,500 lakini orodha inaonyesha kuwa kuna jumla ya 15,500

RAIS Uhuru Kenyatta amewekewa mtego na wakuu serikalini na wafanyabiashara wakubwa ambao wanafanya kila juhudi kuhakikisha wamepata hatimiliki za ploti walizopata kwa njia za ulaghai katika shamba la Embakasi Ranching.

Njama ya wakuu hao, walioko serikalini na waliostaafu na wanaoshirikisha maafisa wa juu serikalini, utawala, usalama na wafanyabiashara ni kuhakikisha majina yao yako katika orodha inayotayarishwa na Wizara ya Ardhi ya wenyehisa watakaopewa hatimiliki.

Duru zinasema wanafanya kila juhudi kuhakikisha wana usemi katika shughuli ya kuhalalisha umiliki wa vipande vya ardhi katika shamba hilo la ekari 40,000 viungani mwa jiji la Nairobi.

Kulingana na Katibu wa Wizara ya Ardhi, Dkt Nicholas Muraguri, Rais Kenyatta aliitaka wizara kuhakikisha wenyehisa wamegawiwa ploti zao na kupewa hatimiliki haraka iwezekanavyo. Hii ni kufuatia vilio ambavyo vimekuwa vikimfikia kutoka kwa wenyehisa.

Uchunguzi umebaini kuwa njama ya kuingilia shughuli hiyo inashirikisha baadhi ya watu kati ya 2,500 walionunua hisa katika kampuni hiyo kwa njia za ulaghai kisha wakajitwalia ardhi katika mashamba ya kampuni hiyo. Wenyehisa wengine 13,000 ndio waanzilishi wa kampuni hiyo lakini hawana usemi.

 

Walagai waingiwa na wasiwasi

Hatua ya Rais Kenyatta kutaka wenyehisa halali wapewe mashamba yao imewatia wasiwasi waliopata hisa kwa njia za mkato kutokana na hofu kuwa huenda wakapoteza ardhi waliyonyakua iwapo agizo hilo litatekelezwa kikamilifu, kwa uwazi na haki. Wengi wao tayari wamejenga kwenye ploti hizo.

Rais Kenyatta alikuwa amepangiwa kutoa hatimiliki kwa wenyehisa mnamo Februari 1 mwaka huu lakini hilo halikufanyika. Hii ni baada ya kufahamika wenyehisa halali walikuwa wamepanga kuandamana siku hiyo kwa kile walihofia ni wamiliki wasio halali kunufaika.

Dkt Muraguri anasema anafahamu kuhusu njama za kuvuruga shughuli ya kuhalalisha umiliki. “Tunashughulikia hilo kwa umakinifu zaidi na tumefungua ofisi ya kupokea malalamishi ya wenyehisa. Pia, tumetwaa orodha ya wenyehisa kutoka kwa kampuni hiyo ya Embakasi Ranching ili kubaini wenye hisa halali.

“Hatuna jingine ila tu kuvunja kampuni hii ili mtindo wa utapeli ambao umekuwa ukiendelezwa ukomeshwe. Ni mpango ambao tutaufanikisha kwa umakinifu na wenyehisa halali watapata haki yao, na wale ambao waliingia katika mradi huu kwa njia ya magendo watapoteza,” akasema Dkt Muraguri.

Kwa mujibu wa msemaji wa wenyehisa wa mradi huo, Joseph Njenga, sababu kuu ya matatizo ya uhalalishaji wa umiliki ulioagizwa na Rais Kenyatta ni kuwa wale ambao walinunua hisa kwa ulaghai wanahudumu katika ngazi za juu serikalini.

 

‘Wezi wamo serikalini’

“Walioiba mashamba yetu wamo serikalini na wana ushawishi mkubwa. Wanafanya kila mbinu kuhakikisha wao ndio watakaonufaika na mpango wa kuhalalisha umiliki wa ardhi. Wanamweka Rais kwenye mtego wa kuidhinisha ulaghai wa mashamba,” alisema Bw Njenga.

Mradi wa Embakasi ulianzishwa 1978 kwa lengo la kilimo cha matunda na mboga na ufugaji ng’ombe. Lakini mnamo 1990 uligeuzwa kuwa kampuni ya uuzaji mashamba kupitia hisa.

“Wakurugenzi walianza kuuza ploti kwa matajiri huku nyingine zikinyakuliwa na wakuu serikalini. Wenyehisa halali wanafaa kuwa 13,500 lakini orodha inaonyesha kuwa kuna jumla ya 15,500,” asema Bw Njenga.

Anasema kuwa hisa iliyompa mnunuzi uhalali wa kumiliki robo ya ekari ya ardhi katika mradi huo ilikuwa ikiuzwa kwa Sh4,000 na kufikia 1990 ikaamuliwa kuwa kila mwenyehisa angepewa ploti moja ya ziada.

“Hapo ndipo ukora ulipoanza kuingizwa na wakurugenzi, ambapo wenyehisa wasio na ufahamu, wale waliokuwa wameaga na pia wale ambao hawakuwa wakifuatilia kwa makini shughuli za kampuni walipokonywa ploti zao na zikauzwa,” asema Njenga.

 

Kubadilishwa kwa ploti

Anasema kuwa hali iliendelea kuwa mbaya zaidi ambapo maeneo ya umma katika mradi huo yalianza kuuzwa huku wanyehisa halali wakibadilishiwa ploti zao zilizokuwa katika meneo ya bei za juu na kusukumwa ndani kwa maeneo ya bei za chini.

Katika hatua inayoonekana kama njia ya kuchelewesha shughuli hiyo, wakurugenzi wa kampuni hiyo wametaka kila mwenyehisa kulipa Sh25,000 za hatimiliki.

Lakini Dkt Muraguri amekashifu wakurugenzi hao na kuwataka wakome kudai pesa hizo akisema kuwa serikali itagharamia utoaji wa hati hizo na pia huduma za usoroveya.

Hata hivyo, wakurugenzi hao wakiongozwa na Mwenyekiti, Thuita Mwangi bado hawajapunguza kiwango hicho, wakisema kuwa kampuni hiyo ni ya kibinafsi.
Kulingana na Bw Thuita, wakurugenzi hao wanatathmini agizo la Dkt Muraguri.

Mmoja wa wenyehisa Bi Mary Wambui, ambaye ni mjane wa aliyekuwa Mbunge wa Starehe Bw Muhuri Muchiri alieleza Taifa Leo kuwa amepokonywa ploti tano. Anasema wenyehisa wana wasiwasi kwani kuna hatari ya wanyakuzi kutumia hila kupata hatimiliki huku wenyehisa halali wakikosa.