Uhuru atetea uhusiano wake na ‘Baba’

Uhuru atetea uhusiano wake na ‘Baba’

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Rais Uhuru Kenyatta ametetea ukuruba kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga huku akipuuzilia madai kuwa uhusiano huo unalenga kuvunja Jubilee.

Rais Kenyatta pia alisisitiza kuwa handisheki kati yake na Bw Odinga haina uhusiano wowote za siasa za urithi 2022 bali inalenga kuhakikisha amani na maridhiano yanadumu nchini kwa lengo la kufanikisha maendeleo.

Akiongea katika kongamano kuhusu miundomsingi katika ukumbi wa Bomas, Rais Kenyatta alisema hawajawahi kujadili ndoto zao za kisiasa au za mwanasiasa yeyote yule.

“Hatujawahi kujadili masuala ya ODM au Jubilee. Haja yetu kuu imekuwa kujadili masuala ambayo yataunganisha taifa hili na kufanikisha malengo yake kimaendeleo,” Rais Kenyatta akasema.

Akaongeza: “Sijui ODM ni nini na wala hatujawahi kujadili kuhusu maswala ya vyama vingine”

Rais Kenyatta alisema Bw Odinga hajawahi kumwambia kuwa anataka kuwania urais 2022 na yeye pia hajawahi kumwambia kiongozi huyo wa ODM kwamba atataka kuendelea kushikilia wadhifa huo wa urais mwaka huo.

“Hajaniambia anataka kuwa Rais 2022; na sijamwambia ninataka kuwa rais 2022. Tumekuwa tu tukijadili masuala yanayowaathiri watu wetu. Ikiwa ni miundo mbinu, tumekuwa tukijadili kile ambacho tunapaswa kufanya kujenga barabara zaidi. Tunajadili, tunasaidiana na kukubaliana,” Rais Kenyatta akasema.

“Ikiwa ni masuala ya afya, huwa ananielekeza kile kuhusu kile ambacho tunapaswa kufanya. Sisi huketi, kujadiliana na kukubaliana. Yeye pia hunipa mawaidha kuhusu jinsi ya kuimarisha kile ambacho tunafanya. Sasa kuna kosa gani hapo? Rais Kenyatta akauliza.

Alisema mustakabali wa wananchi na taifa la Kenya kwa jumla ndio nguzo muhimu inayohimili muafaka kati yake na Bw Odinga.

Rais Kenyatta alisema hayo alipohutubu wakati wa kukamilika kwa mkutano wa kwanza wa miundo msingi barani Afrika kwa jina “Afro Champions Boma Forum on African Infrastructure Financing and Delivery.”

Kauli ya Rais Kenyatta imefasiriwa kama inayolenga naibu wake William Ruto na wabunge wanaompigia debe kuwa kurithi kiti cha urais 2022. Rais anatarajiwa kustaafu katika siasa mwaka hii.

Dkt Ruto na wenzake wamekuwa wakidai kuwa Raila anatumia handisheki kama kisingizio cha kuleta migawanyiko katika Jubilee.

You can share this post!

AKILIMALI: Licha ya ulemavu wake, yuko mstari wa mbele...

BONGO LA BIASHARA: Sh100 za chama kila wiki zajengea...

adminleo