Uhuru ateua majaji saba wapya katika mahakama ya rufaa

Uhuru ateua majaji saba wapya katika mahakama ya rufaa

NA CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ameteua majaji saba wapya katika Mahakama ya Rufaa ambao walipendekezwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

Saba hao ni majaji Luka Kimaru Kiprotich, Lydia Achode, John Mativo na Fredrick Ochieng’.

Wengine ni majaji Grace Ngenye, Abida Ali Aroni na wakili Paul Mwaniki.

Wanasheria hao waliorodheshwa na JSC baada ya kukamilika kwa shughuli ya kuwahoji jumla ya watu 63 waliotuma maombi ya nafasi hizo na kualikwa kupigwa msasa na tume hiyo.

Shughuli hiyo ya mahojiano ilikamilika mnamo Julai 13, mwaka huu chini ya uenyekitiwa wa Jaji Mkuu Martha Koome.

Majina ya majaji hao wapya yaliodheshwa katika Gazeti rasmi la Serikali toleo la Julai 19, na hivyo kuongeza idadi ya majaji katika Mahakama ya Rufaa hadi 26.

Kulingana na sheria, Mahakama ya Rufaa inapaswa kuwa na jumla ya majaji 30.

Kuteuliwa kwa majaji wapya saba sasa kunamaanisha kuwa mahakama hiyo ingali ina pengo la majaji sita.

“China ya mamlaka iliyoko katika Kipengele cha 166 (1) (b) cha Katiba ya Kenya, Miye Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya nawateua Kimaru Luka Kiprotich, Gachoka Paul Mwaniki, Achode Lydia Awino, na Ochieng Frederick Andago, Mativo John Mutinga, Ngenye Grace Wangui na Aroni Abida Ali kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa,” inasema notisi ya gazeti hilo iliyotiwa saini na Rais Kenyatta.

Tangazo hilo limejiri wiki moja baada ya JSC kuwasilisha majina ya saba hao kwa Rais mnamo Julai 13, saa kadha baada ya kukamilishwa kwa mahojiano.

Jaji Mkuu Koome alisema majaji hasa waliteuliwa baada ya kuzingatiwa kwa vigezo vilivyowekwa wakati wa mahojiano yaliyoanza Juni 27.

“Baada ya kuchunguza kwa kima ufaafu wa wale wote waliohojiwa na kwa kuzingatia hitaji la Katiba la ufaafu, jinsia, usawa wa kimaeneo, kitendo sawazishi na masilahi ya umma, JSC inapendekeza uteuzi wao,” Bi Koome akasema katika taarifa iliyowasilishwa kwa Rais Kenyatta.

Mwaka jana, Rais alikataa kuwateua majaji sita ambao waliidhinishwa kuhudumu katika Mahakama ya Rufaa alitaja utovu wa maadili kama sababu.

Majaji hao walikuwa; Profesa Joel Ngugi, George Odunga, Welkon Korir na Aggrey Muchelule, ambao alidinda kuwapandisha vyeo kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.

Pia alikataa kuwateua majaji Judith Omange na Evans Makori kuhudumu kama majaji katika Mahakama ya Mazingira.

  • Tags

You can share this post!

Msanii wa nyimbo za injili anayesaidia watoto mitaani

Wajackoyah atishia kususia mdahalo

T L