Habari

Uhuru ateua mzee mwingine

October 24th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA na SAM KIPLAGAT

RAIS Uhuru Kenyatta amependekeza mzee mwingine ateuliwe katika cheo cha juu serikalini, huku mahakama ikipiga breki uteuzi wa Bi Mary Wambui kusimamia Mamlaka ya Kitaifa Kuhusu Ajira (NEA).

Kasisi Samuel Kobia, aliye na umri wa miaka 72, ndiye mzee wa majuzi kupendekezwa na Rais Kenyatta kusimamia taasisi ya umma. Rais Kenyatta amejizolea sifa ya kuwapendelea wazee ambao wamestaafu kuhudumu katika vyeo vya juu katika serikali yake.

Kasisi Kobia amependekezwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) kuchukua mahala pa Francis Ole Kaparo amnbaye muda wake wa kuhudumu umefika tamati.

Rais alikuwa amepewa orodha ya watu saba ili aweze kuteua mmoja wao, ndiposa akaamua kuendeleza mtindo wake wa kupendelea wakongwe waliokula chumvi nyingi.

Walioachwa nje ni Kenneth Marende (63), Francis Sigei, Michael M. Ndung’u (69), Abdirahman Hassan (58), Humphrey K. Njuguna (58) na Amina Abdallah (50).

Rais pia amemteua mwanasiasa mkongwe Philip Okundi, 77, kuhudumu kwenye bodi ya tume hiyo ya NCIC pamoja na Bw Samuel Kona, Bi Peris Nyutu, aliyekuwa Mbunge wa Mandera Abdulaziz Ali Farah, Bi Fatuma Tabwara, aliyekuwa waziri wa fedha katika Kaunti ya Nairobi Danvas Makori na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Vihiga Bi Dorcas Kedogo.

Majina hayo sasa yatawasilishwa kwa Bunge la Kitaifa ili yapigwe msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Uwiano na Usawa inayoongozwa na Mbunge wa wa Kuteuliwa, Maina Kamanda ambaye ni baba mkwe wa Bw Makori.

Kasisi Kobia ni mhubiri wa Kanisa la Kimethodisti na Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni (WCC) ambako alihudumu kati ya 2004 hadi 2009. Pia alihudumu akiwa Kamishna katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) kati ya 2013 na 2015 kabla ya kujiuzulu ghafla.

Wakati huo huo, Mahakama ya Ajira na Masuala ya Leba imeagiza kuwa Bi Wambui, ambaye ni mbunge wa zamani wa Othaya asianza kazi hadi kesi iliyowasilishwa kupinga uteuzi wake isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Hellen Wasilwa aliitaja kesi hiyo kuwa ya dharura na kusema kuwa itasikizwa Novemba 14

Agizo hilo linatokana na malalamishi yaliyowasilishwa na Chama cha Wabunge Vijana (KYPA), kikisema kuwa kulingana na sheria, Bi Wambui hajatimiza viwango vinavyohitajika kuhudumu kwenye wadhifa huo.

Miaka saba

Chama hicho kilisema kuwa kulingana na masharti yaliyopo, anayeteuliwa anapaswa kuwa amehudumu kwa takribani miaka saba katika kitengo cha kuwasimamia wafanyakazi katika sekta ya umma ama sekta binafsi.

Kilisema kuwa uteuzi wa Bi Wambui unakiuka kipengele cha kanuni za uajiri kwenye mamlaka hiyo.

Kwenye malalamishi hayo, chama hicho kinaeleza kuwa mara kadhaa Bi Wambui amekiri hadharani kwamba hana elimu ya kutosha, hali inayomzuia kuhudumu katika nafasi hiyo.

Kilisema kuwa mshahara ambao Bi Wambui atakuwa akipokea utakuwa sawa na kuwapunja walipa ushuru kutokana na majukumu muhimu ambayo hutekelezwa na mamlaka hiyo.

“Uteuzi wa mtu ambaye hajatimiza viwango vinavyohitajika ni sawa na kukiuka kanuni kuhusu maadili na uongozi,” KYPA kikasema.