Uhuru atia doa ndoa ya ODM, Jubilee

Uhuru atia doa ndoa ya ODM, Jubilee

Na BENSON MATHEKA 

JUKUMU ambalo Rais Uhuru Kenyatta atatekeleza baada ya chama chake cha Jubilee kuungana na ODM linatishia kulemaza muungano wa vyama hivyo viwili vikubwa nchini.

Duru zinasema kwamba, wanachama wa vyama hivyo hawafurahishwi na pendekezo la waandalizi wa mkataba wa muungano huo linalompatia Rais Kenyatta usemi mkubwa hata akiondoka mamlakani baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Ingawa maafisa wakuu wa vyama hivyo wanasema mchakato wa kusuka muungano haujakamilika, duru kutoka Jubilee na ODM zinasema kuna pendekezo la Rais Kenyatta na Bw Odinga kufanya maamuzi ya mwisho kuhusu masuala muhimu wakiungana.

Rais Kenyatta ameonyesha ishara kwamba Bw Odinga ndiye chaguo la mrithi wake na kuungana kwa vyama vyao kunanuiwa kuimarisha kampeni za waziri mkuu huyo wa zamani na kuvutia ufuasi katika eneo la Mlima Kenya.

Huku washirika wa Bw Odinga wakihofia kuwa iwapo Rais Kenyatta atakuwa na usemi mkubwa kwenye muungano wa chama chao cha ODM na Jubilee, ushawishi wa kiongozi wa chama chao utapungua akishinda urais na kuingia mamlakani ilhali wale wa Jubilee wanahisi atawazuia kukwea ngazi kisiasa.

“Ni kweli hiyo hofu iko na tunajaribu kuepuka hali ambapo ‘baba’ akishinda atakaliwa chapati na mtu aliyestaafu. Hata hivyo, uwezo wetu sio mkubwa kwa sababu ni vinara wote wawili wanaoongoza mchakato wa kusuka muungano,” alisema mbunge mmoja wa ODM ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Rais Kenyatta amenukuliwa mara kadhaa akisema kwamba, hana nia ya kukwamilia mamlakani muhula wake ukikamilika baada ya uchaguzi mkuu ujao.

Mnamo Ijumaa, gazeti la People Daily liliripoti kwamba, jukumu atakalotekeleza Rais Kenyatta linatishia kusambaratisha muungano wa vyama vya Jubilee na ODM.

Kulingana na gazeti hilo, suala hilo pia linaweza kuathiri kampeni za Bw Odinga ambazo zimeshika kasi kote nchini chini ya kauli mbiu yake ya Azimio la Umoja.

“Miongoni mwa masuala tata katika mazungumzo ya mapendekezo ni kwamba, Rais Kenyatta na Bw Odinga wasimamie kamati ya juu ya muungano huo na hii imezua utata kwa kuwa iwapo kiongozi wa chama chetu atakuwa rais, itamaanisha hatakuwa na nguvu za kuamua mambo binafsi,” alieleza mbunge huyo.

Washirika wa Rais Kenyatta hasa kutoka eneo la Mlima Kenya nao wanahisi hawatakuwa na nafasi ya kujijenga iwapo Rais Kenyatta ataendelea kuwa na usemi muungano wa Jubilee na ODM ukifaulu kuunda serikali ijayo.

Ni suala tata hivi, kwamba washirika wa Rais wanaounga handisheki yake na Bw Odinga walikataa tutaje majina yao.

“Tunamheshimu Rais lakini tuna wasiwasi kwamba, hafai kuwa akitufanyia maamuzi baada yake kustaafu mwaka ujao 2022. Tunahitaji damu mpya katika uongozi eneo la Mlima Kenya. Tungefurahia akiwa mshauri wetu baada ya kustaafu,” alisema mbunge mmoja kutoka Kaunti ya Nyeri.

Kulingana na Naibu Kiongozi wa chama cha ODM Wycliffe Oparanya, kamati ya wataalamu inayotayarisha muungano wa chama hicho cha chungwa na Jubilee haijakamilisha kazi yake.

“Kamati ya kiufundi iliyotwikwa jukumu la kutayarisha mkataba iko katika awamu ya mwisho. Itakapokamilisha kazi yake, Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga watatangaza muungano,” alisema Bw Oparanya.

Kulingana na wadadisi wa siasa, huenda Rais Kenyatta anatumia mbinu za mlezi wake wa kisiasa, Daniel Moi aliyejaribu kukwamilia katika uongozi wa chama cha Kanu baada ya kustaafu 2002.

“Kuna uwezekano anaiga Rais Moi ambaye baada ya kustaafu 2002, alikwamilia katika uongozi wa Kanu na kuzuia wanasiasa wa Rift Valley kukitumia kujijenga kisiasa. Moi hakuwa amemwandaa mwanasiasa yeyote kumrithi kuwa msemaji wa eneo la Rift Valley kisiasa anavyofanya Rais Kenyatta ambaye hajakuza mrithi wake eneo la Mlima Kenya,” asema mchanganuzi wa siasa, David Osambwa.

You can share this post!

Ruto kusalia Naibu hata akifurushwa Jubilee – Wataalam

Polisi asema atamlipa aliyeumwa na mbwa Sh150 pekee si elfu...

T L