Uhuru atikisa demokrasia

Uhuru atikisa demokrasia

Na WANDERI KAMAU

KENYA imo kwenye hatari ya kuzama kidemokrasia ikiwa Rais Uhuru Kenyatta na washirika wake hawatakoma kuhujumu idara huru za kukuza na kudhibiti utawala wa kisheria.

Wakosoaji wanasema ikiwa Rais Kenyatta atafanikiwa kulemaza Idara ya hakama kama alivyotishia akihutubia taifa siku ya Madaraka Dei mnamo Jumanne, basi atakuwa amefanikiwa kurejesha Kenya katika enzi za udikteta.

Tayari Rais Kenyatta amefanikiwa kudhibiti taasisi zingine muhimu katika kulinda utawala wa kidemokrasia kama vile Bunge, Seneti, Upinzani, vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za umma.

Wadadisi na wataalamu wa masuala ya sheria wamekosoa vikali kauli ya Rais Kenyatta ya kutoa vitisho kwa majaji, wakisema hana haki hata kidogo kuamulia Mahakama utaratibu wake wa kufanya kazi.

“Ni kinaya kwa Rais Kenyatta kuanza kulalamika vile maamuzi ya mahakama yanavyoathiri nchi kiuchumi, ilhali yeye ndiye chanzo kikuu cha hali mbaya ya uchumi nchini.

“Kwa mfano, serikali imekuwa ikifanya kila iwezalo kuwalazimisha Wakenya kukubali BBI licha ya utaratibu mzima kuendeshwa kinyume cha Katiba. Anapaswa kujilaumu mwenyewe,” asema Dkt Barack Muluka, ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa.

“Vitisho dhidi ya taasisi huru ni kuturejesha katika enzi ya chama kimoja. Lazima Wakenya wasimame kidete kutetea Katiba na mafanikio yote tuliyopata kutokana na juhudi za wazalendo waliojitolea maisha yao kuipata Katiba mpya,” akasema Kiongozi wa Narc-Kenya, Martha Karua kwenye mahojiano Jumatano.

Kauli yake inawiana na hisia za mwanaharakati Ndung’u Wainaina, anayetaja vitisho vya Rais Kenyatta kama “urejeo wa udikteta.”

“Vitendo vya Rais Kenyatta vinaonyesha yeye ni kiongozi ambaye nia yake ni kuendelea kukwamilia mamlakani,” akasema Bw Wainaina, ambaye ndiye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kimataifa cha Utatuzi wa Migogoro (ICPC).

Mbunge Rigathi Gachagua wa Mathira, anasema Rais Kenyatta ataacha historia mbaya iwapo hatajitolea kulinda Katiba.

“Ninamfahamu kwa undani Rais Kenyatta kwani nishawahi kuwa msaidizi wake wa kibinafsi. Namshauri kuzingatia Katiba na kuheshimu taasisi huru ikiwa anataka kukumbukwa na vizazi vijavyo,” akasema mbunge huyo.

TAASISI KUHUJUMU SERIKALI

Hata hivyo, watetezi wa Rais Kenyatta wanakosoa vikali taasisi zinazohujumiwa na serikali, wakisema kuna haja ya kudhibiti uhuru wazo.

“Hatuwezi kuwa na taasisi ambazo zinahatarisha uthabiti wa nchi kwa kisingizio cha kuendeleza uhuru wake. Matakwa ya wananchi lazima yazingatiwe na taasisi yoyote ile inapofanya maamuzi,” akasema Mbunge wa Kieni, Kanini Kega.

Mwenzake Ngunjiri Wambugu wa Nyeri Mjini naye aliwataja wakosoaji wa rais kama “wabinafsi.”:

“Wanasiasa na wanaharakati ambao wanamkosoa rais ni watu wanaojali maslahi yao pekee. Lengo lao ni kuvuruga utendakazi wa serikali ili baadaye kupata nafasi ya kumkosoa rais kwa kutotimiza malengo yake,” akasema Bw Wambugu kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Ingawa kulikuwa na matumaini kuwa Idara ya Mahakama ingefungua ukurasa mpya baada ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome majuzi, azma hiyo ilididimia Jumanne baada ya Kiongozi wa Taifa kuikashifu vikali na kuipa vitisho kwa maamuzi ambayo hayamfurahishi ikiwemo kuhusu BBI.

Hatua hiyo inaendeleza mtindo wake wa kudunisha Idara ya Mahakama, ambao amefanikisha kwa kupuuza maamuzi ya majaji na mahakimu.

Jumanne, Rais Kenyatta alifufua uhasama wake na mahakama kwa kurejelea hatua ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali uchaguzi mkuu wa 2017.

Kwenye hotuba yake jijini Kisumu, Rais Kenyatta aliikashifu vikali idara hiyo, akiitaja kuwa “kikwazo katika kuwawezesha Wakenya kuendeleza haki yao ya kufanyia mabadiliko Katiba kupitia BBI.”

Mbali na kurukia mahakama kwa kuzima BBI, Rais Kenyatta amekuwa mkali dhidi ya yeyote anayejaribu kumkosoa, wakiwemo wabunge na maseneta walio na maoni tofauti na yake.

Miongoni mwao ni Seneta Irungu Kang’ata (Murang’a), aliyekuwa Kiranja wa Wengi kwenye Seneti, Mbunge Aden Duale (Garissa Mjini) aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) aliyekuwa Kiranja wa Wengi Bungeni.

Katika juhudi za kuzima sauti huru, serikali vile vile haijazisaza vyombo vya habari na mashirika ya kutetea haki za umma.

Vita dhidi ya vyombo vya habari vilianza baada ya serikali kubuni Mamlaka ya Kudhibiti Matangazo (GAA).

Ingawa serikali ilidai lengo la kubuni mamlaka hiyo lilikuwa kulainisha utaratibu wa utoaji matangazo ya kibiashara ya taasisi za serikali, mamlaka hiyo imelaumiwa kwa kutumia matangazo kunyamazisha kudhibiti vyombo vya habari.

Vyombo vya habari vimekuwa vikilalamika kuhusu kutolipwa mamilioni ya pesa, hali ambayo inatatiza ustawi wa uanahabari nchini.

You can share this post!

Washukiwa 12 wa genge la Wakali Kwanza wajisalimisha

Mwanamke afa kwa ‘hofu ya kukamatwa na polisi’ Kilifi