Habari MsetoSiasa

Uhuru aungana na familia ya mzee Moi kuomboleza

April 22nd, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta ameihakikishia familia ya Rais Mstaafu Daniel Moi kwamba serikali itashirikiana nayo kwenye maandalizi ya mazishi ya marehemu Jonathan Moi, aliyefariki mnamo Jumamosi.

Rais alitoa kauli hiyo jana, wakati alimtembelea Mzee Moi nyumbani kwake, Kabarak, katika Kaunti ya Nakuru.

Kulingana na taarifa kutoka kwa familia hiyo, Rais aliwasili huko mwendo wa saa saba adhuhuri na kupokewa na Seneta Gideon Moi wa Baringo.

Kwenye mazungumzo yao, Rais alimfariji Mzee Moi, huku akimhakikishia ushirikiano wa serikali katika kila hatua ya shughuli za maandalizi ya mazishi ya mwanawe.

“Rais Kenyatta aliwasilisha rambirambi zake na kuihakikishia familia msaada wa serikali kwa kila hatua,” ikasema familia kwenye taarifa.

Kulikuwa na ulinzi mkali saa chache kabla ya Rais Kenyatta kuwasili, huku watu wachache tu wakiruhusiwa kuingia. Polisi wa kikosi cha GSU walikuwa wakipiga doria katika lango kuu na maeneo mengine. Kulingana na taarifa, kikao kati ya Rais Kenyatta na Mzee Moi kilidumu chini ya saa moja.

Ni watu wa familia ya Mzee Moi, washirika wa kanisa la AIC na viongozi kadhaa wa kidini walioruhusiwa kuingia.

Jonathan alifariki mnamo Jumamosi baada ya kuugua saratani kwa muda mrefu akiwa na umri wa miaka 65. Alizaliwa mnamo Julai, 23, 1954.

Watoto wengine wa Mzee Moi ni:

Jennifer Chemutai Kositany: Ndiye kifungua mimba wa Mzee Moi. Alizaliwa mnamo 1953. Alisomea katika Shule ya Msingi ya Kenya High School, ambapo baadaye alielekea nchini Amerika kwa masomo zaidi. Huwa anaishi maisha ya faragha. Mumewe alifariki katika ajali mnamo 1994.

John Mark: Ni mojawapo wa wanawe Mzee Moi ambao huishi maisha ya siri sana. Alizaliwa mnamo 1958. Alikuwa mwerevu masomoni, ikilinganishwa na wenzake, hali iliyomfanya kupata ufadhili wa masomo katika Chuo Kikuu cha Harvard, nchini Amerika. Hata hivyo, alirudi nchini bila kumaliza masomo yake.

Raymod Kipruto Moi: Alizaliwa mnamo 1960 na anafahamika sana alipohudumu kama naibu mwenyekiti wa Shirika la Kununua Maziwa (KCC) katika miaka ya tisini. Kwa sasa ndiye mbunge wa Rongai.

Philip Kipchirchir Moi: Alihudumu katika jeshi, ambapo kwa sasa ni afisa mstaafu wa jeshi. Amekuwa akigonga katika vichwa vya habari kwa miaka mitano iliyopita kutokana na mzozo kati yake na mkewe, Rosanna Pluda. Bi Pluda ni raia wa Italia.

Vile vile, anajulikana kwa kuwa mshiriki wa Mashindano ya Mchezo wa Gofu ya Ngong.

Doris Elizabeth Chepkorir Choge: Ni pacha wa Philip. Alizaliwa mnamo 1962. Amekuwa akiishi maisha ya kisiri. Awali, Mzee Moi alipinga ndoa yake kwa Ibrahim Choge, mwanawe mwanasiasa mkongwe Simon Kiptum. Mumewe alifariki mnamo 1998 katika ajali ya barabarani.

June Moi: Alisomea katika Shule ya Msingi ya Nairobi, Shule ya Upili ya Kenya High na baadaye akaelekea nchini Canada kupata elimu ya chuo kikuu. Kinyume na dada zake, anajihusisha sana katika masuala ya biashara.