Habari MsetoKimataifaSiasa

Uhuru avumisha Kenya Airways nchini Amerika

September 25th, 2018 2 min read

Na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta alianza shughuli za kikazi jijini New York, Marekani Jumapili kwa kukutana na wafanyabiashara mashuhuri na wakuu wa makampuni wakati wa karamu ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na shirika la ndege la Kenya Airways kwa maandalizi ya kuzindua safari za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi New York mnamo tarehe 28 Oktoba.

Rais Kenyatta, ambaye yuko New York kwa mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA), alilipongeza shirika la ndege la Kenya Airways na washirika wake kwa kutia bidii kutimiza safari za moja kwa moja kati ya Kenya na Marekani.

“Kwa niaba ya Wakenya, naishukuru Serikali ya Marekani kwa kushirikiana nasi kutekeleza wazo hili,” kasema Rais Kenyatta wakati wa karamu ya chakula cha jioni iliyofanyiwa katika jingo la Rockefeller Plaza lililoko jijini New York.

Wafanyabiashara mashuhuri wa safari za ndege na waekezaji waliohudhuria sherehe hiyo walihimizwa kushirikiana ili kuharakisha uekezaji wa Marekani nchini Kenya ambapo safari hizo mpya za ndege za moja kwa moja zitafungua ukurasa mpya wa kuboresha utalii, biashara na uekezaji.

Alitoa wito kwa Wakenya wanaoishi Marekani kutumia fursa ya safari za ndege za moja kwa moja ambazo zinapunguza kwa kiasi kikubwa gharama na muda wa safari hizo kupitia nchi nyingine za Ulaya.

Rais Kenyatta aliishukuru Serikali ya Marekani kwa kutoa fursa kwa Kenya Airways kushiriki katika mpango wa Ushauri wa masuala ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka.

“Mpango huo utatoa mafunzo na usaidizi wa kiufundi kwa mashirika yanayohusika na masuala ya usimamizi wa forodha na mipaka ambayo yatashughulikia safari za moja kwa moja za shirika la ndege la Kenya Airways kwenda nchini Marekani,” kasema Rais Kenyatta.

Aliongeza kwamba serikali yake imeimarisha uekezaji katika miundomsingi ya safari za ndege ili kuiwezesha sekta hiyo kutimiza jukumu lake muhimu katika kustawisha uchumi wa Kenya na kushirikisha uchukuzi wa abiria na mizigo katika mataifa mengine ya Afrika na Ulimwengu.

Shirika la Ndege la Kenya Airways litakuwa na safari za kila siku kutoka Nairobi kwenda New York na vile vile kutoka New York kuja Nairobi.

Tayari abiria wapatao 7,000 wamejiandikisha kutumia ndege hizo zitakazozinduliwa tarehe 28 mwezi Oktoba.

Usafiri huo utakuwa wa haraka kati ya Afrika Mashariki na New York, huku ndege hizo zikitumia muda wa masaa 15 kwenda jijini New York na masaa 14 kuja Nairobi.

Shirika la Ndege la Kenya Airways litakuwa la kwanza kabisa kutoa huduma hizo za safari za moja kwa moja kutoka Afrika Mashariki na Marekani.

Mwenyekiti wa shirika la Ndege la Kenya Airways Michael Joseph na Mkurugenzi Mkuu Sebastian Mikosz walimshukuru Rais Kenyatta kwa kuunga mkono shirika hilo katika kutimiza malengo yake.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kihistoria ni Mawaziri Monica Juma (Mashauri ya Kigeni), Peter Munya (Viwanda) na Katibu Mkuu wa Uchukuzi Esther Koimet miongoni mwa wageni wengine mashuhuri.