Habari

Uhuru awafinya mawakili

July 18th, 2020 2 min read

BENSON MATHEKA na VALENTINE OBARA

MAWAKILI wamepata pigo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuagiza mashirika ya serikali yasipeane kandarasi za huduma za uwakili kwa mawakili wa kibinafsi bila kushauriana na Mwanasheria Mkuu.

Imebainika kuwa, mashirika hayo pia yaliagizwa kuondoa kesi zote dhidi ya idara za serikali.

Agizo hilo lilitolewa wiki iliyopita wakati Rais Kenyatta alifanya mkutano na mawaziri, manaibu wao na makatibu wa wizara.

Kwa mujibu wa arafa iliyochapishwa na Waziri wa Usalama wa Nchi Fred Matiang’i, wakuu wa mashirika na idara za serikali walipewa siku 21 wafutilie mbali maelewano kati ya idara zao na mawakili wa kibinafsi ambao walikuwa wamepewa kazi bila idhini ya Mwanasheria Mkuu, Kihara Kariuki.

Ingawa hatua hii inaonekana kulenga kupunguza gharama za matumizi ya fedha serikalini, mawakili walilalamika kwamba ni dhuluma kwa taaluma yao.

Vitengo vya serikali hutumia mamilioni ya pesa kugharamia huduma za mawakili wa kibinafsi, hasa vinapokumbwa na kesi mahakamani.

“Kumkabidhi Mwanasheria Mkuu mamlaka haramu ili aamue mawakili wanaofaa kuwakilisha asasi za serikali kutasababisha ufisadi na mapendeleo ya kikabila,” wakili Ahmednasir Abdullahi alilalamika katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Ilifichuka baadhi ya taasisi za serikali zilikuwa tayari zimearifiwa na mawaziri kuhusu agizo hilo.

Arafa iliyotolewa na Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha, kwa taasisi za umma za elimu ilionyesha kuwa, mbali na agizo hilo, Rais Kenyatta aliagiza pia mashirika yote ya serikali na taasisi za umma ziondoe kesi ambazo zinahusu idara nyingine za serikali.

Profesa Magoha alisema hii ni kufuatia agizo la Rais Kenyatta ambalo lilitaka kesi hizo ziondolewe katika muda wa siku saba.

Uhusiano kati ya Chama cha Mawakili wa Kenya (LSK) na Afisi ya Rais haujakuwa mzuri kwa muda sasa.

Mwezi uliopita, LSK ilienda kortini kumshtaki Rais kwa madai kuwa anajaribu kubadili mfumo wa usimamizi wa mahakama kinyume cha sheria.

LSK pia ilijaribu kuwaondoa Mwanasheria Mkuu Kihara na Wakili Mkuu wa Serikali Ken Ogeto, kutoka kwa orodha ya mawakili kufuatia mzozo ambapo Rais hajaidhinisha majina 41 ya majaji wapya.

Hata hivyo, wawili hao waliokolewa walipoenda Mahakama Kuu ambayo ilizuia hatua hiyo kwa muda.

Katika mkutano wake na mawaziri, Rais Kenyatta pia aliagiza idara na mashirika ya serikali kutoanzisha miradi mipya kabla ya kukamilisha ile inayoendelea.

Rais aliwataka wakuu wote wa mashirika na vyuo kutembelea miradi iliyo chini yao na kukutana na wananchi ili wajue kwamba serikali inafanya kazi alivyoagiza.

Vile vile, taasisi za umma zilitakiwa kuhakikisha zimekamilisha kulipa madeni yaliyotokana na utoaji huduma na bidhaa kutoka kwa makampuni mbalimbali.

Wawekezaji ambao walipata kandarasi kwa taasisi za umma wamekuwa wakilalamika kuhusu kucheleweshwa malipo yao na kuwafanya wafilisike kibiashara.