Habari

Uhuru akutana na madiwani wa Nairobi kujadili utoaji huduma

February 29th, 2020 1 min read

COLLINS OMULO na PSCU

RAIS Uhuru Kenyatta amekutana na madiwani wote wa Chama cha Jubilee (JP) katika Kaunti ya Nairobi katika Ikulu kujadili utoaji huduma serikali kuu ikijiandaa kuchukua baadhi ya majukumu.

Katika mkutano huo wa Jumamosi masuala ya mshikamano wa kitaifa na vita dhidi ya ufisadi pia vimejadiliwa.

Hatua hiyo inajiri siku chache kabla ya kuwasilishwa kwa hoja ya kumng’atua Gavana Mike Sonko uongozini.

Hoja imepangiwa kuwasilishwa Jumanne ijayo.

Awali, walikuwa wamepokea mwaliko.

“Mnafahamishwa kwamba tuna mkutano kesho (leo Jumamosi) katika Ikulu kuanzia saa tatu asubuhi. Nawaomba muwe mmefika kufikia saa 2.45 asubuhi,” ikasema taarifa kutoka kwa Kiranja wa Wengi Bi June Ndegwa kwa madiwani.

Duru zilisema kuwa mkutano huo unalenga kutafuta muafaka kuhusu mpango huo, ikizingatiwa hoja hiyo inaendeshwa na madiwani wa Upinzani.

“Madiwani wengi wa Jubilee walikuwa tayari kuunga mkono hoja hiyo. Ninajua kwamba tutaelezwa kutounga mkono hoja itakapowasilishwa,” akasema diwani ambaye hakutaka kutajwa.

Hilo linajiri siku chache baada ya mkutano mwingine katika Ikulu, ambapo Bw Sonko aliyakabidhi baadhi ya majukumu yake kwa Serikali ya Kitaifa.

Kwenye mwafaka huo, Bw Sonko aliikabidhi Serikali majukumu manne makuu, ambayo itaanza kuyasimamia Machi.

Duru ziliiambia ‘Taifa Leo’ kuwa kwenye mkutano wa Jumanne, Rais Kenyatta aliondoa uwezekano wowote wa uchaguzi mdogo jijini, baada ya kupata ushauri kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.