Uhuru awapuuza wanaotilia shaka utendakazi wake

Uhuru awapuuza wanaotilia shaka utendakazi wake

VALENTINE OBARA na ANTHONY KITIMO

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali wakosoaji wake wanaotilia shaka utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya utawala wake.

Akiwa katika Kaunti ya Mombasa wikendi, Rais alisema serikali yake imetekeleza miradi mingi inayonufaisha maisha ya wananchi kama vile ujenzi wa miundomsingi ya uchukuzi na usambazaji umeme mashinani.

“Yale ambayo tunafanya ni kwa sababu tunataka kuona nchi yetu ikisonga mbele na ikipata maendeleo. Tumemaliza tatizo la watu kujihisi wamesahaulika na serikali yao. Tunataka kila Mkenya mahali popote alipo, ajiskie ni Mkenya na serikali yake inamsaidia kwa mahitaji yake,” akasema Rais Kenyatta.

Ijapokuwa aliepuka kutaja mwanasiasa yeyote kwa jina, matamshi yake yalionekana kulenga yale yaliyosemwa na naibu wake awali.

Katika mahojiano kwenye runinga mwishoni mwa wiki iliyopita, Dkt Ruto alisema serikali ilifanikiwa kutekeleza miradi mingi katika kipindi cha kwanza kulichodumu kati ya 2013 hadi 2017.

Alidai kuwa, katika kipindi cha pili kilichoanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2017, serikali ilikuwa imelenga kufanikisha miradi chini ya Ajenda Nne za maendeleo lakini lengo hilo likatatizwa na siasa za handisheki.

Alipohutubia hafla ya kuzindua mpango wa Sh10 bilioni wa kustawisha uvuvi Pwani, Rais Kenyatta alisisitiza bado yuko mamlakani hadi mwaka ujao akataka wengine wasubiri wakati wao ufike, akikisiwa kumlenga naibu rais.

“Kwa wale ambao wanataka kuendelea kupiga nduru, wapige. Sisi tuko kazini mpaka dakika ya mwisho na haja yetu ni kuhakikisha taifa la Kenya litakuwa bora zaidi kuliko ilivyokuwa. Wale ambao watakuja baadaye pia wataendelea na kazi,” akasema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Pwani wakiwemo Magavana Ali Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi), Salim Mvurya (Kwale), Dadho Godhana (Tana River) na Fahim Twaha (Lamu) kando na wabunge na maseneta kutoka ukanda huo.

Rais alimwagiza Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani, aharakishe utoaji wa fedha za kufadhili miradi ili ikamilishwe kabla astaafu urais mwaka ujao.

Jumatano iliyopita, Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) liliidhinisha mkopo wa dola milioni 407 (Sh43.9 bilioni) kwa serikali ili kupiga jeki ukosefu wa fedha katika bajeti ya kitaifa ya mwaka huu.

Wakati huo huo, Rais Kenyatta alionekana kukashifu mtindo wa kisiasa wa naibu wake ambaye amekuwa akigawa vifaa vya kikazi kwa makundi ya vijana na wanawake.

“Kazi na jasho ndiyo itakusaidia. Hawa wanakuambia mambo ya bure ni… wacha nisiseme sijakuja kuongea hayo maneno,” akasema, huku akikosoa baadhi ya viongozi kwa kutusi wenzao kila wanapohutubia umma.

Rais na naibu wake wamekuwa wakitoa misimamo tofauti kuhusu masuala mbalimbali ya kiserikali, licha ya kuwa wao ndio wameshika usukani wa uongozi.

Uhasama wao ulianza mwaka wa 2018 punde baada ya Rais Kenyatta na Bw Odinga kuweka mwafaka wa ushirikiano.

Tofauti zao zilizidi katika miezi ya hivi majuzi baada ya rais kuashiria ataungana na Bw Odinga katika uchaguzi wa mwaka ujao, huku vyama vya ODM na Jubilee vikiendeleza mipango ya kuunda muungano wa kisiasa.

  • Tags

You can share this post!

Ukambi: Wazazi wahimizwa wakumbatie chanjo

Shujaa na Lionesses watiwa katika makundi ya kifo ya...